Simu janja kutumika kulinda hifadhi za bahari Z’bar

Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imeanza mpango wa kulinda na kusimamia maeneo matano ya hifadhi ya bahari kwa kutumia mfumo maalumu uliounganishwa katika simu janja.

Hatua hiyo imekuja baada ya wizara hiyo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kuhifadhi Wanyamapori (WCS), kugawa simu zilizounganishwa kimfumo kwa wasimamizi wa maeneo hayo Unguja na Pemba.

Hifadhi hizo tano ni Chabamca, Tumca, Peca, Mimca na Minai.

 Wakati wa kugawa vifaa hivyo leo Jumapili Mei 26, 2024, Meneja wa Hifadhi ya Minai, Dk Thani Rashid amesema lengo la mkakati huo ni kusaidia ukusanyaji wa taarifa wakati wa ufanyaji wa doria ili kudhibiti matumizi yasiokubalika kisheria ya hifadhi za bahari.

 “Simu hizi zinauwezo wa kuchukua takwimu katika mazingira ya bahari ikiwemo aina ya chombo na uvuvi, aina ya zana zinazotumika baharini na nani anayefanya shughuli hiyo pamoja na kuchukuliwa hatua kwa wakati stahiki,” amesema Dk Thani.

 Naye ofisa kutoka WCS, Yussuf Said Yussuf amesema kutokana na muundo wa simu hizo haziruhusu matumizi ya mitandao ya kijamii hivyo kuwataka watumiaji kujiepusha na jambo hilo.

 “Tuzitendee haki katika matumizi yake kufikia lengo na mafanikio kudhibiti matumizi mabaya katika uhifadhi wa bahari,” amesema.

Amesema mategemeo ni kufungua fursa zaidi kupitia ukusanyaji wa taarifa muhimu ambazo zitasaidia katika kufanya maamuzi pamoja na kuonesha aina ya shughuli zinazofanyika katika hifadhi za bahari.

 Akizungumza kwa niaba ya wasimamizi wa hifadhi za bahari Zanzibar, Amour Mussa Juma amesema kupitia vifaa hivyo na mafunzo waliopatiwa wapo tayari kutekekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

 Amesema vifaa hivyo vya kisaa vitawasaidia katika majukumu yao na kurahisisha kazi zao kwani awali walikuwa wakitumia karatasi jambo ambalo lilikuwa halina ufansi kutokana na mazingira ya bahari wakati mwingine hupotea.

 “Tumekabidhiwa vifaa hivi ambavyo tulikuwa tukivililia siku nyingi kwa ajili ya kuendeleza doria za baharini ili kupambana na uvuvi haramu kwa lengo la kuendeleza uhifadhi wa bahari,” amesema.

Related Posts