Straika mpya Simba ambakiza Freddy, ajiaandaa na maisha mapya Msimbazi

Kikosi cha Simba bado kipo jijini Arusha kwa ajili ya pambano la mwisho la Ligi Kuu Bara ili kujua hatma ya ushiriki wa timu hiyo katika mechi za kimataifa msimu ujao kama itaenda Ligi ya Mabingwa au itaangukia Kombe la Shirikisho Afrika, lakini huku nyuma straika mpya aliyebakisha hatua chache kutua Msimbazi amezuia kutemwa kwa Freddy Michael kikosini akitaka aje kucheza naye ili wagawe dozi kwa wapinzani.

Mshambuliaji huyo aliyetaka Freddy aliyesajiliwa dirisha dogo la msimu huu na kufunga mabao sita hadi sasa ni Ricky Banda ambaye amekiri Simba imebakiza hatua za kumalizia dili la kutua Msimbazi, lakini akamtaja Freddy kati ya wachezaji wa sasa wa kikosi hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Banda alisema kwa sasa anajiandaa kwa maisha mapya nje ya Red Arrows ya Zambia baada ya kufikia sehemu nzuri ya kumalizana na mabosi wa klabu hiyo.

Banda aliyefunga mabao 10 hadia sasa katika Ligi Kuu ya Zambia ikiwa ni bao moja na yale aliyofunga Freddy wakati akiwa nchini humo na kikosi cha Green Eagles, alisema Simba ni klabu kubwa na ameshajianda kiakili kuipigania klabu hiyo yenye mashabiki wenye presha kubwa ya matokeo.

“Nadhani tuwasubiri Simba wenyewe waamue kwa sasa naendelea na mechi za kumalizia msimu hapa Arrows (Red), kuna malengo ya timu na malengo yangu binafsi napambana kuyafikia,” alisema Banda na kuongeza;

“Ninachoweza kukwambia ni nimeshajiandaa kwenda kucheza soka la ushindani zaidi nje ya Zambia, ofa nilizonazo zote ni kubwa lakini hii ya Simba naiona ni kubwa zaidi kwa kuwa nataka kucheza kwenye ligi au timu yenye mashabiki wenye presha kubwa ya kutamani matokeo mazuri.

Mbali na Simba, Mwanaspoti linafahamu kuwa Zesco ya Zambia nayo inapigana kuinasa saini ya straika huyo anayejua kufunga kwa staili zote vichwa na miguu yote.

Aidha, Banda aliongeza kuwa hana mashaka na kiwango cha mshambuliaji Freddy Kouablan aliyesajiliwa na Simba akitokea ligi ya nchini humo akisema jamaa atakiwasha tu akizoea sawasawa.

“Koublan (Freddy) ni mshambuliaji mzuri sana, alipokuwa hapa amethibitisha ubora wake, unaweza kuona namna ambavyo tunapambana kuzima rekodi yake ya kufunga wakati akiwa hayupo hapa.

“Nadhani kama atabaki tutafanya vizuri sana tukikutana hapo kama mambo yatakamilika, kuna wakati sisi washambuliaji mabao yanachelewa lakini baadaye hali huwa inatulia.”

Simba imekuwa ikihaha kusaka mshambuliaji anayejua kufunga kutokana na John Bocco kugeukia ukocha huku ikiachana na Jean Baleke na Moses Phiri aliyerudi Zambia na kuwaleta Freddy na Omar Pa Jobe ambao hata hivyo wameshindwa kukonga nyoyo za mashabiki hadi sasa wakati timu ikishika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara na kutolewa katika michuano ya Kombe ya Shirikisho (FA).

Related Posts