VIVUKO KIGAMBONI: Bomu linalosubiri kuingiza nchi kwenye maafa

Dar/mikoani. Usalama wa zaidi ya watu 60,000 wanaotumia huduma ya vivuko kati ya Kigamboni na Magogoni kila siku upo shakani.

Mashaka ya usalama wa watu hao yanatokana na ubovu wa vivuko hivyo, unaosababishwa na kutofanyiwa matengenezo makubwa kwa mujibu wa sheria, ratiba na matakwa ya kitaalamu.

Hali hiyo inazua hofu ya kuharibika vivuko hivyo vikiwa safarini, kama ilivyowahi kutokea mara kadhaa vyombo hivyo vilipozima vikiwa na abiria katikati ya maji.

Abiria wakifanya malipo tayari kuingia kwenye vivuko vya Magogoni – Kigamboni

Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), kwa siku ni zaidi ya abiria 60,000 wanaohudumiwa na vivuko vya Magogoni-Kigamboni.

Uchunguzi wa gazeti la Mwananchi, umebaini vivuko hivyo aghalabu hupitiliza muda wa matengenezo makubwa, jambo ambalo ndiyo msingi wa uhai na ufanisi wake.

Sheria ya Usalama wa Vyombo vya Majini (Solas) ya mwaka 1974 inataka matengenezo makubwa ya vivuko vinavyotumika kwenye maji ya bahari yasizidi miaka mitano.

Matengenezo hayo kwa mujibu wa sheria hiyo, pia yanapaswa kufanyika chini ya miaka mitano, kwa maelekezo ya mamlaka ya udhibiti wa huduma za majini ya nchi husika, baada ya kujiridhisha na ubovu wa kivuko husika.

Mbali na matakwa ya kisheria, taarifa ya ubora wa vivuko (sea worthiness) inaeleza injini za vivuko hivyo (Mv Kigamboni, Mv Kazi na Mv Magogoni), zinapaswa kubadilishwa mara tu zitakapofanya kazi kwa saa 10,000.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebainika ukiukwaji wa sheria ya Solas ya mwaka 1974, kwa kuwa baadhi ya vivuko vinavyotoa huduma Kigamboni vimefikisha miaka sita bila kufanyiwa matengenezo makubwa, huku vikiendelea kufanya kazi, Mv Kigamboni kikiwa miongoni mwa hivyo.

Kwa mujibu wa ratiba ya matengenezo (nakala tunayo), Mv Magogoni kilipaswa kufanyiwa matengenezo makubwa mwanzoni mwa mwaka 2023, lakini hadi sasa hayajafanyika.

Hata hivyo, Mwananchi limearifiwa juu ya Wakala wa Huduma za Meli (Tasac) kusitisha huduma za kivuko hicho ili kulinda usalama wa watumiaji, lakini bado kipo kazini kinatoa huduma.

“Inashindikana kutekelezeka kutokana na uhalisia wa mahitaji, abiria ni wengi kuliko idadi ya vivuko inalazimika kitumike vivyo hivyo,” anaeleza mmoja wa maofisa wa Temesa, kwa sharti la kutotajwa jina.

Mv Kazi kilifanyiwa matengenezo makubwa mwaka 2022 injini zake zikiwa zimefanya kazi saa 24,000, ambazo ni mara mbili na zaidi ya matakwa ya kitaalamu.

Mv Magogoni ambacho kwa sasa kipo kwenye matengenezo, kilipelekwa Februari, 2023 lakini hadi kinapelekwa kilishapitiliza muda wa matengenezo kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kutokana na hali hiyo, kumekuwa na matukio kadhaa ya vivuko hivyo ama kuyumbishwa na upepo kwa urahisi au kuzima vikiwa na abiria katikati ya maji.

Januari 25, 2023 kivuko cha Mv Kigamboni kilizima katikati ya maji na kulazimika kuvutwa kwa kamba.

Hali kama hiyo ilitokea Mei 12, 2023 kwa kivuko hicho, pia Septemba 18, mwaka jana.

Kutozingatiwa sheria, ratiba na matakwa ya kitaalamu kuhusu matengenezo makubwa ya vivuko hivyo, kunachangiwa na kukosekana fedha za kutekeleza kazi hiyo, kama inavyofafanuliwa na chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Serikali.

Chanzo hicho kilichozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina, kinasema matengenezo makubwa ya vivuko hugharimiwa na Serikali Kuu kupitia bajeti za mwaka.

Bajeti hizo, anasema huwa na vipaumbele lukuki na kutolewa kwake huwa kwa kusuasua.

Hilo limethibitishwa kupitia mpango wa matengenezo ya kivuko cha Mv Kigamboni unaotaka bajeti itolewe katika mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 30.

Licha ya mpango wa matengenezo kutaka hayo, mwaka huu wa fedha ukikaribia kufika mwisho, hakuna kiasi chochote cha fedha kilichotolewa au mkataba na mkandarasi uliosainiwa.

“Hakuna fedha ndiyo sababu matengenezo hayafanyiki, mpango upo lakini Serikali ina vipaumbele vingi, hadi matengenezo yafikiwe muda umeshapita,” kinaeleza chanzo hicho.

Kama haitoshi, bajeti pia inakwamisha kukamilika matengenezo makubwa ya kivuko cha Mv Magogoni.

Kivuko hicho kilipelekwa nchini Kenya, Februari mwaka jana kwa matengenezo yaliyotarajiwa kukamilika kwa miezi sita, yaani hadi Agosti, 2023.

Lakini uhalisia tangu kivuko hicho kipelekwe nchini humo, imeshapita miezi 15 bila matengenezo kukamilika na hakina dalili ya kurejea nchini mwaka huu.

Uchunguzi umebaini mkwamo huo unasababishwa na Serikali kutokamilisha malipo ya mkandarasi kwa ajili ya matengenezo ya kivuko hicho.

Malipo ya awali yaliyopaswa kufanywa tangu Februari 2023, lakini yamefanyika Februari 2024.

Malipo yaliyofanyika Februari ni asilimia 10 ya Sh7.5 bilioni ambayo mkandarasi African Marine and General Engineering Company Ltd anapaswa kulipwa.

Ofisa wa ngazi ya juu kutoka kampuni hiyo ya Mombasa nchini Kenya, aliliambia Mwananchi kuwa, hadi sasa ni kazi za awali tu ndizo zilizoanza kufanyika.

Anaeleza matengenezo hayo yalipaswa kuanza kivuko kilipofika karakana, lakini ilishindikana kwa kuwa Serikali ya Tanzania haikuwa imelipa.

“Matengenezo yanahitaji vipuli na vifaa vingine ambavyo African Marine and General Engineering Company Ltd inapaswa kuviagiza kwa fedha, kama hakuna fedha zilizolipwa, inakuwa si rahisi kuanza kazi,” anasema ofisa huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, malipo ya awali yaliyopaswa kufanyika mwaka jana, ndiyo yamelipwa Februari 2024.

“Kazi zimeanza lakini zile za awali na matengenezo yale yanahitaji kubadilisha kila kitu, zikiwemo injini nne, kwa hiyo hatujafikia hata kuagiza injini, suala ambalo ni mchakato unaochukua zaidi ya miezi sita,” anasema.

Kutokana na mazingira hayo, Mv Magogoni iliyotarajiwa kurejea Agosti, 2023 haina dalili za kurejea nchini hata mwaka huu utakapoisha.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kalahala amesema shughuli zinaendelea na kivuko kitarejea (bila kuweka wazi ni lini).

Kuhusu kusuasua kwa malipo ya mkandarasi, hakuwa tayari kulifafanua, akisisitiza Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha kazi hiyo inatekelezwa.

“Serikali inafanya kila namna kuhakikisha matengenezo yanafanyika ili kivuko kirejee na wananchi waendelee kupata huduma,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu vivuko kuchelewa kupelekwa kwenye matengenezo, Kilahala amekiri kuwepo kwa hali hiyo, akifafanua kuwa inasababishwa na mpangilio wa ratiba bila kuathiri huduma kwa wananchi.

Anasema baada ya kivuko cha Mv Magogoni kurejea kutoka kwenye matengenezo (haijulikani ni lini), Mv Kigamboni kitapelekwa kupata huduma hiyo.

“Matengenezo yamefanyika kwa kupishana, mpango wetu ni Mv Magogoni itakaporudi, Mv Kigamboni itakwenda kwenye matengenezo,” anasisitiza.

Meneja wa Ujenzi na Matengenezo ya Vivuko wa Temesa, Lukombe King’ombe anasema kwa sababu mahitaji ya huduma za vivuko ni makubwa, hatua ya kuvipeleka kwa matengenezo makubwa inafanyika bila kuathiri huduma hizo.

Kwa sababu ya wingi wa mahitaji, anasema ni vigumu kutoa vivuko vyote kwa pamoja kuvipeleka kwenye matengenezo.

Anaeleza, wanalazimika kupeleka kimoja wakati vingine vikiendelea kutoa huduma.

“Kuna idadi kubwa ya watu ambao maisha yao ya kila siku ni kuvuka kwa ajili ya kwenda Kariakoo na Posta kutafuta riziki, hii ndiyo inayofanya tusivipeleke vyote kwenye matengenezo makubwa,” anasema. Itaendelea kesho

Related Posts