Liwale. Wakazi 1,428 wa Kijiji cha Nangano kilichopo Wilaya ya Liwale mkoani Lindi wanarajiwa kunufaika na mradi wa maji wa Sh461 milioni unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa).
Akizungumza leo Jumapili Mei 26, 2024 mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava, Meneja wa Ruwasa Liwale, Ruhumbika Wegoro amesema mradi huo utanufaisha wakazi 1,428 na hadi sasa umebaki asilimia chache kukamilika.
Wegoro amesema mradi huo utaanza kutumika Mei 30, 2024 na wananchi wameamua kuchangia Sh30 kwa ndoo moja ya maji ili kuendeleza mradi.
“Mradi utahudumia wananchi 1,428 na umegharimu Sh450 milioni na ujazo wake ni lita 50,000. Mradi huu utasaidia kumaliza kero ya maji ya kijijini hapa iliyodumu kwa muda mrefu,” amesema Wegoro.
Kiongozi wa mbio za mwenge, Mnzava baada ya kukagua mradi huo na kuweka jiwe la msingi, amewataka wananchi kutunza mazingira na kuacha uharibifu kwenye vyanzo vya maji na miundombinu.
“Ninachotaka wananchi wapate majisafi na salama, niwaombe wananchi kutunza vyanzo vya maji pamoja na jumuiya ya watumia maji kuwa walinzi namba moja, nisisitize yeyote atakayehujumu miundombinu ya maji akigundulika achukuliwe hatua,” amesema Mnzava.
Hata hivyo, Mnzava ameipongeza Wilaya ya Liwale kwa kuanza kutekeleza mfumo mpya wa ununuzi unaoepusha matumizi mabaya ya fedha.
“Hawa Ruwasa wamefanya vizuri kwa kutumia mfumo mpya wa ununuzi unaosaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia rushwa na kuongeza wigo kwa wazabuni, niwatake halmashauri zingine kutekeleza matumizi ya mfumo huu kwa mujibu wa utaratibu na kisheria,” amesema Mnzava.
Mkazi wa Nangano, Zainabu Salim ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo kwenye kijiji chao akisema walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta maji.
“Tulikuwa tunatembea umbali mrefu kufuata maji, lakini baada ya kujengewa na watu wa Ruwasa, tunashukuru adha inakwisha, tunaishukuru sana Serikali kutuona sisi watu wa Nangano,” amesema Zainabu.
Jumla ya miradi saba wilayani Liwale yenye thamani ya Sh2.4 bilioni imetembelewa, kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi.