Pemba. Wananchi wa Mji wa Machomane Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba, wametakiwa kushirikiana na viongozi wa dini kurejesha maadili kwa vijana, yanayotajwa kuporomoka.
Kiongozi wa Jumuiya ya Kiislamu Jai, Shekh Khamis Mwadini ametoa kauli hiyo leo Jumapili Mei 26, 2024 wakati akizungumza na wananchi hao katika mkutano wa kujadili mporomoko wa maadili unavyouathiri mji huo.
Amesema kumekuwa kukijitokeza vitendo viovu vinavofanywa na baadhi ya vijana, jambo ambao linaweza kusababisha kutokea kwa vitendo vya kihalifu.
Amesema wananchi wanapaswa kuungana katika kukomesha vitendo hivyo, kama vile zinaa, ambayo im ewaathiri vijana wengi.
“Niwaombeni wananchi wa Mji wa Machomane, tushirikiane turudishe maadili, tunaona vitendo viovu vinavojitokeza, vijana wanavuta bangi, zinaa na hata wizi, tunapaswa tusimame imara kupiga vita vitendo hivyo,” amesema.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi hao kuzidisha malezi ya pamoja katika kuwajengea misingi ya maadili mema watoto wao kwa kuwasomesha vitabu vitukufu vya dini.
Kwa upande wake Mlezi wa Jumuiya ya hiyo, Subira Khamis Faki amesema Mji wa Machomane ndio wenye wageni, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kurejesha maadili.
Hata hivyo amewaomba wananchi hao kujenga utamaduni wa kusaidia wenye matatizo mbalimbali kama vile wagonjwa.
“Maisha yetu ni kama mnavoyajua, hali za maisha ni ngumu lazima tujenge utamaduni wa kusaidiana kwani kitendo hicho ni miongoni mwa maandiko yanayohimizwa kwenye dini yetu,” amesema.
Sheha wa Shehia ya Wara katika Mji wa Machomane, Massoud Mohamed Khamis amesema katika kuondoa vitendo viovu kwenye mji huo ni lazima wananchi wawe tayari kupambana na kutoa taarifa pindi yanapotokea vitendo vya uvunjwaji wa maadili.
“Kuna vitendo huwa vinajitokeza kama wizi, udhalilishaji, inawekana jamii inavifumbia macho mkihofia muhali, naomba tuondoshe muhali vichukuliwe hatua ili jamii iweze kuwa salama,” amesema Masoud.