Zaidi ya watu 8,000 wamehama hifadhi ya Ngorongoro

Ngorongoro. Serikali imesema hadi sasa kaya 1,373 zenye jumla ya watu 8,364 waliokuwa na makazi ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wamehama kwa hiari kutoka eneo hilo na kwenda Msomera na maeneo mengine nchini.

Vilevile, imeeleza kuwa haijasitisha baadhi ya huduma muhimu zikiwemo za elimu na afya katika maeneo ambayo bado wananchi wake hawajaondoka.

Hayo yamebainishwa leo Mei 26, 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mpango wa uhamaji wa hiari kutoka eneo hilo.

Amesema katika awamu ya kwanza iliyoanza Juni 16, 2022 hadi Januari 18, 2023, jumla ya kaya 551 zenye watu 3,010 zilihama,  kaya 503 zenye watu 2,692 zikihamia Msomera na 48 zenye watu 318 kwenye maeneo mengine ya nchi, katika mikoa zaidi ya minane na kaya hizo zote zilikuwa na mifugo 15,321.

Amesema awamu ya pili iliyoanza Agosti 24, 2023 hadi Aprili 28, 2023, ilihusisha kaya 822 zenye watu 5,354zilizohama, kati yake 745 zenye watu 4,855 zilienda Msomera na 77 zenye watu 499 zilienda maeneo mengine ya nchi na idadi ya mifugo iliyohama na wananchi hao ni 21,136,

“Katika awamu zote mbili tangu mpango huo uanze, kaya 1,373 zenye watu 8,364 zimeshahama ambapo Kijiji cha Msomera hadi kimepokea kaya 1,248 zenye watu 7,547 na maeneo mengine kaya 125 zenye watu 81.

“Jumla ya mifugo iliyohamishwa ni 36,457, kati ya hiyo 30,314 imeenda Msomera na 6,143 kwenye maeneo mengine nchini,” ameongeza Matinyi.

Akizungumzia madai ya baaadhi ya wananchi waliohama kutoka eneo hilo kutolipwa fidia wala stahiki zao, Matinyi amesema siyo ya kweli na kuwa shughuli ya uhamaji hufanyika baada ya malipo ya fidia kukamilika.

“Wanahama wakishavunja makazi au maendelezo na kuchagua mali wanazotaka kuhama nazo, hapo ndipo usafirishaji wa watu, mifugo na mali zao hufanyika kwa hiari na kwa kuhakikisha wasafiri.

“Kuna ‘clip’ zinasambazwa na watu walioamua kutibua ukweli wa suala hili, ila kinachofanyika kila mkuu wa kaya hupewa stahiki zote, ndipo wanahama.

“Kwa wanaohamia maeneo mengine ya nchi mbali ya usafiri wa kuhamia, hulipwa hela za ziada Sh10 milioni kwa wanaohamia Msomera, Saunyi na Kitwai na Sh15 milioni kwa wanaohamia maeneo mengine ya nchini,” amesema.

Amesema huduma za wananchi wanaoendelea kubaki zinaendelea katika eneo hilo wakati uhamasishaji na elimu vikiendelea ili wahame, katika baadhi ya maeneo zitapungua ikiwemo kutokuongeza madarasa katika vijiji ambavyo wananchi wake wanaendelea kuhama.

“Huduma hazijasitishwa, Serikali inabeba jukumu la kuwahudumia lakini kadri watu wanavyopungua baadhi ya vitu vitapungua.

“Nikitolea mfano shule za msingi mwaka 2023 katika kata 11 zinatakiwa kuhama kwa hiari katika eneo hili, wamepelekewa walimu 22 ila katika wilaya ya Temeke yenye wananchi zaidi ya milioni 1.5 ilipelekewa mwalimu mmoja, mtu anayesema Serikali haitoi huduma inabidi awe mwangalifu,” amesema.

Kuhusu madai ya baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi katika Kijiji cha Msomera kudai kuondolewa katika eneo hilo bila kulipwa fidia, amesema wananchi hao walikuwa wamevamia eneo hilo lililokuwa Pori Tengefu na haikuwaondo,  badala yake iliwapa hati miliki na kuwaacha waendelee kuishi na kufanya shughuli zao.

Amesema wakazi zaidi ya 100,000 wanatarajiwa kuhama katika eneo hilo na mpango wa Serikali ni kujenga nyumba 5,000, kati ya hizo, 2,500 zitajengwa katika kijiji cha Msomera, 1,500 Kitwaina na 1,000 zitajengwa Saunyi.

Hadi sasa nyumba 1,000 zimekamilika Msomera na kati ya hizo, 737 zinakaliwa na watu huku nyingine 263 zikiwa tayari na zinazubiri kuanza kupokea kaya nyingine kuanzia wiki ijayo.

Akizungumzia hali ya utalii, Matinyi amesema NCAA imeendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi kwa kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori aina ya faru ambao ni adimu pamoja na kupambana na kudhibiti mimea vamizi na kuimarisha nyanda za malisho kwa ajili ya wanyamapori.

Amesema NCAA imeendelea kupokea idadi kubwa ya watalii ambapo kati ya Julai 2023 hadi Aprili 2024, imepokea watalii 780,281 huku idadi ya mapato yaliyotokana na watalii hao yakiongezeka hadi kufikia Sh188.5 bilioni na kuvuka lengo la Sh155.4 bilioni. Idadi ya wageni waliofika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 wamefikia 752,000.

Related Posts