Aliyekuwa kocha Simba afikisha siku 553 rumande 

Aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultani (40) na wenzake wanaendelea kusota rumande kwa siku 553 sasa, kutokana na upelelezi wa shauri lao kutokamilka.

Sultan na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Novemba 21, 2022 na kusomewa mashtaka yao.

Hata hivyo, tangu wafikishwe mahakamani hapo siku hiyo, hadi leo Jumatatu Mei 27, 2024, washtakiwa hao wamefikisha siku 553, sawa na mwaka mmoja na miezi sita, wakiwa rumande kutokana upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Licha ya upelelezi wa kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 71/2022 kutokukamilika, pia washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande, kutokana na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Vilevile,  mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili washtakiwa hao, hayana  dhamana kwa mujibu wa sheria.
Leo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga aliieleza mahakama hiyo, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo Serikali inaomba  mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mwanga alitoa taarifa hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Lyamula alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 10, 2024, itakapotajwa na washtakiwa wapo rumande kutoka kesi hiyo kutokuwa na dhamana.

Washtakiwa hao wanatetewa na wakili Daudi Mzeri na  kesi hiyo ilisikilizwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa rumande.

Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa Kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif; Said Matwiko mkazi Magole; Maulid Mzungu maarufu Mbonde(54) mkazi wa Kisemvule ambaye ana undugu na mtuhumiwa Muharami. 

Wengine ni John John maarufu Chipanda(40), mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph.

Awali washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano, lakini Septemba 23, 2023, Mkurugenzi wa mashtaka nchini ( DPP) aliwabadilishia hati ya mashtaka kwa kuwaongezea mengine  matatu likiwemo la kutakatisha fedha na kisha kuwasomea upya mashtaka yao.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kuongoza genge la uhalifu, shtaka linalowakabiliwa watu wote ambapo Inadaiwa  tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti  ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride.

Shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 27.10.

Vile vile, Novemba 4, 2023 washtakiwa, Zuberi, Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa  wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa Kilo 7.79.

Katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa kuwa Aprili 15, 2021 katika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam alinunua magari manne aina  ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies LTD, huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Katika shtaka la nane inadaiwa kuwa Aprili 20,2021, mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies LTD akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
 

Related Posts