Askofu Shoo: Chagueni viongozi wenye hofu ya Mungu

Mtwara. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Fredrick Shoo amewataka Watanzania kuwakataa viongozi wabinafsi hasa wanaowatelekeza wapigakura baada ya kushinda uchaguzi.

Akizungumza kwenye ibada ya kitaifa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya CCT iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mjini Mtwara jana Mei 26, 2024, Askofu Shoo amesema kuwa ni wajibu wa Wakristo kuomba ili wapatikane viongozi wenye hofu ya Mungu.

“Unapochangua mbunge akuwakilishe bungeni, tangu siku anapokanyaga ndani ya Bunge anapotea, makosa unayo wewe uliyemchagua. Tuchague watakaotujali kwa masilahi ya Taifa.

“Kama kuna mbunge umeona jinsi alivyoweka mbele masilahi, yaani tangu 2020 alivyochaguliwa amewasahau na hawajamuona tena, lakini mwaka huu na mwakani utamuona akipita pita kila nyumba, mwambieni hatukujui kama ambavyo wewe hutujui,” amesema.

Amewataka Wakristo kutafuta wacha Mungu bila kujali dini zao na kuwashawishi kugombea uongozi.

“Wajibu wetu ni sisi kuangalia viongozi wa aina gani ambao ni waadilifu na wacha Mungu, wasukumeni hata kuwaambia kuwa ndio wanafaa kuwa viongozi.

“Tuangalie watu waadilifu, usiangalie dini wala madhehebu na wanafahamika kila mahali, watu hao ndio tuwape jukumu la kugombea ili tusiishie kulalamika,” amesema.

Kwa upande wake Kaimu Katibu CCT, Godlisten Moshi amewataka Wakristo kuunga mkono wagombea wenye sifa, ambao watajitokeza katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu, bila kujali vyama vyao, dini wala madhehebu na ushabiki.

 “Unajua tuanapaswa kujiandaa kikamilifu, hasa uchaguzi mkuu kwa kugombea tunapokuwa na sifa, ili tuwapate viongozi wenye sifa na hofu ya Mungu tujitokeze kwa wingi,” amesema Moshi.

Akizungumza katika ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Patrick Sawala amewataka wananchi kujiandaa na mchakato wa uchaguzi.

“Mwaka huu kutakuwa na uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Kupiga Kura na kuhuisha taarifa, tufuatilie jambo hili muhimu ili tujiandikishe na kushiriki.

Aliongeza: “Wakristo tunapaswa tuombeeni uchaguzi ujao uweze kufanyika kwa utulivu na amani na pia uwe wa haki.”

Related Posts