KILE chenye raha huwa kina karaha yake. Shabiki mmoja wa Yanga amejikuta kwenye maumivu ya muda baada ya kutandikwa teke mgongoni na farasi wa Polisi.
Wakati Yanga ikiendelea na msafara wake wa kulitembeza Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ulipofika eneo la Temeke Chang’ombe pale Chuo Cha ufundi Veta shabiki mmoja akamsogelea farasi wa Polisi kwa nyuma katika harakati za furaha yake na kujikuta akipokea teke la nyuma.
Baada ya teke hilo shabiki huyo alianguka chini kwa sekunde Moja kisha kuinuka haraka huku akishika mgongo wake kwa maumivu na kuanza kukimbia taratibu
Baada ya dakika Moja, shabiki huyo akasahau maumivu hayo kisha kuendelea na vaibu lake la kuishangilia ubingwa huo.
Baada ya tukio hilo askari aliyekuwa akimwendesha farasi huyo alimwagia maji mnyama huyo mithili ya kumpoza hasira .
Baada ya kumwagia maji akawataka mashabiki hao kukimbia kwa mbali na Farasi huyo ili kuepusha tukio kama hilo na wote kutii fasta.
Baada ya hapo mashabiki hao walitia adabu na kutomsogelea farasi huyo kila shabiki akiwa makini asimsogelee mnyama huyo na mambo yakaenda vizuri.