Unguja. Licha ya kuipitisha bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walitishia kuizuia bajeti hiyo wakimtaka Waziri mwenye dhamana, Lela Muhamed Mussa kuwapa majibu yanayoridhisha kuhusu ubora wa miundombinu ya elimu.
Maeneo yaliyoibua hoja yalikuwa ni miundombinu, mitalaa, masilahi ya walimu na elimu ya juu, upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kujifunza. Hata hivyo, bajeti hiyo ya Sh830 ilipitishwa.
Katika michango ya wawakilishi hao leo Jumatatu, Mei 27, 2024 licha ya kupewa dakika tano kuchangia tofauti na dakika 15 za kikanuni kutokana na muda, wawakilishi hao licha ya kuonyesha yanayofanywa kwenye elimu lakini walisema mengi hayaendi sawa.
Naibu Spika wa baraza hilo, Mgeni Hassan Juma amesema wizara imeshindwa kuwa na mpango maalumu wa elimu ya watoto wadogo (ECD).
Mgeni amesema kuna shule nyingi za watoto wadogo maarufu ‘day care’ au ‘baby class’ lakini kila mmoja anajiendeshea anavyotaka bila kuwa na miongozo yoyote.
“Tumeshindwa kuwa na sera maalumu za watoto wadogo, hizi shule tena zote ni za binafsi hakuna za Serikali, zinafanya kazi bila miongozo, hili jambo halijulikani lipo wapi wakati kazi ya Serikali ni kutengeneza sera,” amesema.
Amezitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na wizara ya elimu kukaa pamoja na kuwa na mipango ya kutengeza miongozo.
Amesema shule mbadala hazijatiliwa mkazo. Pia kuhusu elimu jumuishi, amesema kuna watoto wanachanganywa lakini hawapewa umuhimu wake, unakuta darasa lina wanafunzi zaidi ya 70 kisha kuna watoto wanne ndio wenye mahitaji maalumu.
Hoja hii pia ilichangiwa na Mwanaasha Khamis Juma mwakilishi wa Dimani ambaye ametaka kujua mafunzo ya namna gani yanayotolewa kwa ajili ya wanafunzi hao na upatikanaji wa vifaa.
Kuhusu mitaala Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Mussa ameonyesha wasiwasi wa ufanisi wake akisema uzoefu unaonyesha kila inapobadilishwa mitalaa kunakuwa na changamoto kwani jambo hilo lazima liende na mabadiliko ya walimu.
“Tusije kutengeneza felia nyingi badala ya kuleta mageuzi kwani ukikosa mfumo wa elimu mzima utakuwa umepwaya,”amesema.
Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Muhamed Ali Suleiman amesema shule zina uchakavu wake licha ya maghorofa yanayojengwa lakini kwenye jimbo lake hakuna hata moja.
Mwakilishi wa Aman, Rukia Omar Ramadhan amehoji walimu kutolipwa posho zao kwa Unguja lakini Pemba wameshalipwa.
Akilijibu suala hilo, Waziri Lela amesema tatizo la kuchelewa kulipa posho kwa walimu wa Unguja ni kutokana na kuwapo kwa udanganyifu.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Elimu, Ali Abdugulam Hussein amesema elimu ni kipaumbele cha kwanza ndio maana wamefanya ongezeko la bajeti kuonyesha dhamira thabiti.
Amesema wanakarabati shule chakavu 100, ujenzi shule za chini 27 na ghorofa zaidi ya 20 na wizara haiwezi kupeleka maghorofa kila eneo ikiwamo kusikokuwa na mahitaji.
Amesema kwa mwaka huu wa fedha wanafunzi 1,000 wataomba mikopo na posho ya vitabu kila mwanafunzi atapata Sh200,000.
Naye Waziri Lela amesema wizara hiyo imeongezewa bajeti kutoka zaidi ya Sh400 bilioni hadi Sh830 bilioni kwa hiyo miundombinu itajengwa japo kwa kuzingatia vipaumbele.
“Haiwezekani kujenga kwa wakati mmoja kwa hiyo kuna vipaumbele hivyo yapo maeneo ambayo yanatakiwa kukarabatiwa hususani yenye hali ngumu,” amesema.
Amesema lengo la Serikali ni kuwa na mkondo mmoja na kila darasa isizidi wanafunzi 45.
Kuhusu kupungua Sh29 bilioni hadi Sh27 bilioni katika bodi ya Mikopo, Waziri Lela amesema kimsingi sio kwamba imepungua ila walibaini wanafunzi wengi walikuwa hawaombi bodi ya mikopo ya Tanzania bara, hivyo kwa bajeti hii wanategemea wapate angalau asilimia tano kwa hiyo itakuwa imeongezeka.