Balozi Nchimbi: Mfumo wa elimu utawasaidia Watanzania kushindana kimataifa

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inafanya mageuzi ya mfumo wa elimu ili kuendana na mahitaji ya nyakati na kuwafanya vijana washindane kimataifa.

Amesema mageuzi hayo yatasaidia vijana wa Kitanzania kumudu changamoto wanazopitia na kuunganishwa kwa ukaribu, kuwania fursa mbalimbali, kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidiplomasia.

Amesema hayo leo Mei 27, 2024 alipokuwa anawahutubia wanafunzi, wazazi na Jumuiya ya Shule ya Dar es Salaam International Academy, akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya kidato cha sita.

“Elimu ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika kutusaidia na kuwajengea msingi imara vijana wetu, hasa wanapopambana kwenye hii dhana ya raia wa kimataifa. Ulimwengu umekuwa mahali padogo na kuzidi kutufanya sisi kuwa raia wa dunia katika nyanja tofauti. Tunapaswa kuwa sehemu ya washiriki washindani si kujitenga,” amesema.

“Tanzania inafanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu kuendana na mahitaji ya kimataifa, kuweka mkazo katika mahitaji ya nyakati za sasa na mbele zaidi ili vijana wetu washindane kimataifa,” amesema

Anasema kasi ya maendeleo ya ulimwengu yanaonyesha ukweli uraia wa nchi yoyote kwa sasa, huwezi kujitenga kwa maana ya kuelewa jinsi unavyofanya kazi, kuthamini utofauti, na kushirikiana kutafuta majawabu ya changamoto na kutumia fursa mbalimbali zilizopo kila mahali.

Vilevile, Balozi Nchimbi amesisitiza licha ya Tanzania kuweka maandalizi ya misingi imara kwa ajili ya watu wake kuwa na uwezo wa kushindana kimataifa,  imejidhatiti kuendelea kuenzi, kuthamini, mila, desturi na tamaduni.

“Tamaduni zetu zimekuwa tunu na utambulisho wa Tanzania na Watanzania katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo katika kushindania fursa i kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake,” amesema.

Mbali na mahafali hayo, shule hiyo mwaka huu imesherehekea miaka 20 tangu ilipoanzishwa.

Related Posts