Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, (wa pili kulia), na Mkurugenzi wa Trademark Africa, Elibariki Shammy, (kushoto) wakisaini mkataba wa mashirikiano kati ya Taasisi hizo Mei 27,2024 Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, (kulia), na Mkurugenzi wa Trademark Africa, Elibariki Shammy, (kushoto) wakionesha hati za mikataba baada ya kusaini Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, akizungumza na waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kumalizika zoezi la kusaini makubaliano hayo.
Mkurugenzi wa Trademark Africa, Elibariki Shammy, (kushoto) akiongea na waandishi wa Habari katika hafla hiyo
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM.
TUME ya Ushindani (FCC), imesaini mkataba wenye thamani ya sh. Bilioni 1.5 na Trademark Africa kwa lengo la kukuza Uchumi wa Biashara nchini na kuimarisha utendaji kazi wa Tume hiyo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, amesema mkataba huo ni wa miaka mitatu, na kwamba ulianza kufanyakazi mwezi Novemba mwaka jana.
Ameeleza kuwa mkataba huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili ambapo mwaka moja wataangalia matokeo yaliyopatikana ndani ya miaka hiyo miwili na kujiridhisha utendaji kazi wake kama ilivyokusudiwa.
Aidha, Erio amesema fedha hizo zitatumika katika mambo matatu yakiwemo kufanya maboresho ya miundombinu ya Tehama, mafunzo kwa wafanyakazi wao na kuwekeza zaidi katika mitandao ya kidigitali.
“Unaweza ukawa na miundombinu mizuri, ukawa na kilakitu kilichokamilika lakini kama watumiaji wa mifumo hawaielewi vyema, ufanisi tunaoutarajia hautakuwepo hivyo tutahakikisha wafanyakazi wa FCC wanapata elimu ya kutosha” amesema Erio.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Trademark Africa, Elibariki Shammy amesema lengo la kushirikiana na FCC ni kuhakikisha eneo la sera linakuwa bora na kutanua wigo mpana wa biashara ngazi ya kimataifa.
“Mkataba huu ni endelevu, kufuatia eneo la sera ya biashara kuwezesha Tanzania kupata fursa ya uwekezaji.
“Dunia inakuwa kwa kasi ndiyo maana tumeshirikiana na FCC katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika soko la biashara na kuwakaribisha wawekezaji,” amesema Shammy.