Macron awakumbuka Wayahudi waliouawa na Manazi – DW – 27.05.2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, aliandamana na mwenyeji wake Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, na viongozi hao walifika kwenye eneo hilo la Makumbusho ya Wayahudi waliouawa hapa barani Ulaya.

Marais wote wawili waliweka mashada ya maua yaliyotengenezwa kwa kutumia rangi za bendera za mataifa yao. Viongozi hao waliandamana na wake zao, mabibi Brigitte Macron mke wa rais wa Ufaransa na bibi Elke Büdenbender mke wa rais wa Ujerumani. Baadae viongozi hao na wake zao walizuru nyumba ya makumbusho.

Soma Zaidi: Rais Macron aanza ziara rasmi ya siku tatu Ujerumani

Takriban Wayahudi milioni 6 waliuawa na Manazi wa Ujerumani barani ulaya kote.

Hapo baadaye, Rais Macron na mkewe wanatarajiwa kwenda kwenye ngome ya Moritzburg iliyo karibu na mji wa Dresden katika jimbo la Saxony mashariki mwa Ujerumani na watasindikizwa na wenyeji wao Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeierna mkewe Elke Büdenbender.

Ziara ya kiserikali ya Rais wa Ufaransa Macron - Berlin
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe walipowasili mjini BerlinPicha: Christophe Gateau/dpa/picture alliance

Macron atatoa hotuba inayotarajiwa kuwa kivutio kikuu katika mji huo wa Dresden ambapo atazungumzia juu ya Sera ya Ulaya mbele ya Kanisa mashuhuri la Frauenkirche. Hotuba itaelekezwa mahsusi kwa vijana wa Ulaya.

Maelfu ya watu kutoka kwenye jimbo la Saxony kutoka Poland, Jamhuri ya Czech na Ufaransa wanatarajiwa kuhudhuria.

Leo Jumatatu ziara ya Rais wa Ufaransa inajumuisha pamoja na kukutana na kufanya majadiliano na wataalamu kwenye Taasisi ya Fraunhofer for Photonic Microsystems iliyopo mjini Dresden ambapo majadiliano hayo yatahusu akili ya kubuni (AI) na viwanda vya kutengeneza teknolojia ya kuhifadhi kumbukumbu kwa kimombo (microchip) hapa barani Ulaya.

Soma Zaidi: Ujerumani Ufaransa na Poland kujadili masuala ya Usalama 

Kesho Jumanne, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, anatarajiwa kuhitimisha ziara yake ya kiserikali kwa kuanzia kwenye chuo kikuu cha Münster katika mji ulio magharibi mwa Ujerumani ambapo atatunukiwa Tuzo ya Amani ya Kimataifa ya Westphalia.

Baadae alasiri Macron atahudhuria mashauriano ya kiserikali kati ya Ufaransa na Ujerumani kwenye Ikulu ya Meseberg, ambayo ni nyumba ya wageni mali ya serikali ya Ujerumani iliyoko kaskazini mwa jiji la Berlin.

Rais Macron ametahadharisha juu kura za maoni zinazopendekeza kuwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinaweza kupata uungwaji mkono zaidi katika uchaguzi ujao wa bunge la Umoja wa Ulaya.

Rais wa Ufaransa I Emanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AP/picture alliance

Ziara ya Macron ni ya kwanza ya kitaifa kufanywa na rais wa Ufaransa katika kipindi cha takriban miaka 25 na inajiri huku nchi mbili zenye nguvu barani Ulaya za Ujerumani na Ufaransa zikiwa zinakabiliana na changamoto kadhaa.

Related Posts