MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemshukia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake ya CCM, (UWT), Mary Chatanda na kusisitiza kuwa kelele wanazompigia ni sawa na kumuwekea mziki unaompa nguvu ili aendelee kuwapiga ‘spana’. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Kauli hiyo ya Makonda imekuja siku mbili baada ya Chatanda kumtuhumu kuwa anadhalilisha watendaji wa serikali.
Akizungumza kwenye semina ya wabunge wa viti maalumu, manaibu waziri, mawaziri, makatibu wa jumuiya ya wazazi ngazi ya mkoa na wilaya jijini Dodoma, Chatanda alisema amewatumia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara Abdulrahmani Kinana kipande cha video ‘clip’ inaonesha Makonda akimdhalilisha mmoja wa watumishi wa mkoa wa Arusha.
“Nimesikitishwa sana na ‘clip’ imezunguka kule Arusha, Longido jana (juzi) haikuwa jambo jema wala sio zuri hata kidogo. Kama wewe ni kiongozi mkuu wa Serikali na umemuona mtendaji wako amekosea, huwezi kuwa na kauli na ulimi usiokuwa mzuri,” alisema Chatanda.
Hata hivyo, akijibu madai hayo leo Jumatatu, Makonda amesema “naomba mvumilie, mtapata watu wengine watawasaidia kuwapetipeti ila kwangu mimi hilo hapana!
Akizungumza baada ya kuwasili katika Wilaya ya Monduli katika ziara yake ya siku sita za moto mkoani humo, amesema “Nasikia kuna watu wanahangaika na mitandao yao ile, ni kama wananipigia rhythm wakati wa kulala.
“Kwa mimi kwa umri huu nitishike na kauli za watu? nawaona kama vile ukiwa kwenye chumba cha massage wakakuwekea kale kamziki … sasa mimi nasikia hiyo hali ya kunipa nguvu ya kuendelea na leo nipo Monduli kuwapiga spana, wavivu wote lazima wanyooke,” amesema Makonda.