Makonda apiga marufuku hospitali kuzuia maiti

Monduli. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amepiga marufuku hospitali za mkoa huo kuzuia maiti kwa sababu ya kushindwa kulipa madeni ya gharama za matibabu.

Amesema kazi ya huduma ya afya ni kazi ya wito ya kumtanguliza Mungu na kuwa katika baadhi ya maeneo wameona kuna changamoto na wanaotuhumiwa ni wataalamu wa afya, wkiwemo wauguzi na madaktari na kuwa katika mkoa huo hataki kusikia malalamiko ya wananchi kutoka kwenye kada hiyo.

Makonda ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Mei 27, 2024, wakati akizungumza na watumishi  katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli, kwenye ziara yake anayoendelea nayo mkoani hapa.

Agizo hilo limewahi kutolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa katika ziara ya Makonda (akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM) mkoani Tanga, Januari 20, 2024, akizitaka hospitali zote za umma kutozuia miili ya marehemu kwa kigezo cha kushindwa kulipa deni la gharama za matibabu.

Akizungumza leo, Makonda amesema ni marufuku kusikia wananchi wanalalamika kwa kunyimwa miili ya ndugu zao kutokana na kushindwa kulipa gharama za matibabu na kuwa Serikali ilishatoa katazo.

“Kwenye huu mkoa ni marufuku kung’ang’ania mwili wa mgonjwa aliyefariki na familia ikashindwa kulipa gharama. Si jambo jema mtu aliyemleta ndugu yake amepambana, mwingine ameuza mpaka shamba, pikipiki mwingine alikuwa ana kibanda ameenda kukopa hadi kwenye Vicoba kabisa, kumuuguza ndugu yake.

“Ndugu yao amefariki wameshindwa kulipa bili, mnabaki na maiti yake siku ya kwanza hadi tatu mpaka anatafuta sehemu nyingine ya kuchangisha mpaka anashindwa kukomboa mwili wa ndugu yake, huu si ubinadamu.

“Mnakwaza imani za watu, ndugu zangu Waislamu wanajua taratibu na imani ilivyo, haiwezekani wanahangaika kuzunguka kuchangishana siku tatu wewe umeng’ang’ania tu maiti, ambayo hata ukiachiwa unaenda kuzika kwa kumtupa ndugu yao kule, tusilete maumivu na mateso,” ameongeza.  

Makonda amesema Mkoa wa Arusha unafaa kuwa mfano wa huduma nzuri za afya ili kuendana na uwekezaji mkubwa wa Serikali, iliyotoa fedha nyingi za kuwezesha miundombinu bora ya utoaji wa huduma za afya.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Hoapitali hiyo, Dk Edward Lengai amezungumzia mradi wa ujenzi unaondelea wa majengo ya mionzi, upasuaji na wagonjwa wa nje, aqmbao umegharimu zaidi ya Sh900 milioni, kuwa utakamilika Juni 15, mwaka huu.

Related Posts