Wizara ya ulinzi ya Niger imesema kuwa mataifa matano ya kanda ya Sahel yamefanya luteka ya kijeshi magharibi mwa Niger. Mazoezi hayo yatakayoendelea hadi mnamo Juni 3 ni ya kwanza ya aina hiyo katika eneo hilo linalokumbwa na hujuma za makundi ya itikadi kali za kiislamu.
Mataifa ya Sahel yatekeleza luteka ya kwanza ya kijeshi
Mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi yanahusisha mataifa matano ya kanda ya Sahel ya — Burkina Faso, Chad, Mali, Niger na Togo. Eneo la Sahel limekuwa likikumbwa kwa miaka mingi na waasi wanaohusishwa na makundi ya kigaidi ya Al-Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu.
“Luteka hiyo inafanyika kitaifa katika kituo cha mafunzo cha kikosi maalum huko Tillia,” wizara ya ulinzi ya Niger imesema kwamba. Luteka hizo zinahusisha “mbinu za kimkakati” na “mipango inayolenga kuimarisha uhusiano kati yao na wakaazi wa eneo hilo”.
Luteka hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika hadi Juni 3 mwaka huu, ni ya kwanza za pamoja za kijeshi kati ya nchi hizo tano.
Mamlaka za kijeshi nchini Burkina Faso, Niger na Mali zimewaondoa wanajeshi kutoka Ufaransa, ambaye ni mtawala wa zamani wa kikoloni, na wanaonekana kuzidi kugeukia Urusi kwa msaada.
Soma zaidi Hatma ya vikosi vya Ufaransa Mali mashakani
Muungano wa mataifa ya sahel unasema nchi hizo zilianzisha mapatano ya ulinzi wa pande zote, na mwezi Februari zilitangaza kujiondoa katika jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS.
Mauaji yashuhudiwa tena Mali
Wakati hayo yakiendelea, Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa itikadi kali wamewauwa takriban raia 20 katikati mwa Mali, katika shambulio la hivi punde katika eneo lililokumbwa na ghasia kwa miaka mingi.
Wakaazi watatu wameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanamgambo hao waliwafyatulia risasi wanakijiji kilomita tatu (chini ya maili mbili) kutoka Diallassagou. Idadi ya watu waliojeruhiwa ni watu 21.
Meya wa Bankass Moulaye Guindo amesema watu wasiojulikana waliokuwa na silaha wamevamia na kuwashambulia wanakijiji waliokuwa wakielekea kufanya kazi katika mashamba yao.
Mapinduzi katika nchi hizo tatu katika miaka ya hivi karibuni yalichochewa na kuzorota kwa hali ya usalama, iliyochangiwa na mzozo wa kibinadamu na kisiasa.