Miili minne yapatikana ajali ya mtumbwi Katavi

Katavi. Miili ya watu wanne kati ya saba wanaohofiwa kufariki dunia kwa ajali ya mtumbwi katika Mto Lunguya uliopo Kitongoji cha Lunguya Kijiji cha Mwamapuli mkoani Katavi imepatikana.

Mtumbwi huo uliokuwa umebeba watu 14 na mizigo ya mazao ulipinduka Mei 26, 2024 ukidaiwa kuzidiwa na uzito na watu saba kuzama majini.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 27, 2024, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe, Silas Rumba akiwa kwenye eneo ilipotokea ajali hiyo amesema juhudi za kuwatafuta waliosalia zinaendelea, kwani vikosi vya uokoaji vipo vinatumia boti kutafuta miili hiyo.

“Uokoaji unaendelea hapa, mpaka sasa tayari miili ya watu wanne imepatikana kati ya saba ambao walifariki kwenye ajali hii na juhudi za kuitafuta mingine mitatu iliyobaki zinaendelea.

“Vikosi vya uokoaji vipo vinaendelea na kazi ya kuwatafuta kwa kutumia boti za kisasa, tunaamini miili iliyobaki itapatikana tu kwa uwezo wa Mungu,” amesema Rumba.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamapuli, John Alfonce amesema ajali hiyo imewasikitisha sana kwani waliopoteza maisha ni nguvu kazi iliyokuwa inatoka kwenye uzalishaji mali wakiwa na magunia 10 ya mpunga.

“Tunaomba Serikali iliangalie hili Kwa makini, kwani maji haya ni mageni kwenye hili eneo, lakini kutokana na Mto Kavuvu kuvunja kingo zake, ndio umesababisha maji hayo kuingia katika kijiji chetu na kuleta madhara kama haya,” amesema.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Inspector Lilian Wanna amesema juhudi za uokoaji zimewesesha kupatikana kwa miili minne.

“Sasa kazi ya kutafuta miili ya watu watatu bado inaendelea tunaomba wananchi waendelee kuwa na subira wakati vikosi vikiendelea kutafuta miili ya ndugu zao,” amesema Wanna.

Related Posts