Mziba arusha jiwe gizani Simba

KITENDO cha Simba kudondosha ubingwa mara tatu mfululizo kimemuibua staa wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba kuhoji usajili unaofanywa na viongozi wa klabu hiyo una manufaa au ni wa mazoea.

Mziba alikuwa akijibu swali la Mwanaspoti aliloulizwa kwa uzoefu wake anadhani Simba inakwama wapi? na majibu yake yalikuwa hivi: “Siwezi kuwalaumu viongozi wa Simba moja kwa moja, ila kupitia  wachezaji wanaowaleta una manufaa gani kwa timu yao au bado wanaendelea kusajili kwa mazoea.

Ameongeza kuwa, “ukweli wa Simba inachokionyesha uwanjani upo kwa viongozi wenyewe. Nachoweza kuwashauri waige mfano wa Rais wa Yanga, injinia Hersi Said ameingia mwenyewe kusajili na tunaona wachezaji aliowaleta wanafanya kazi nzuri.

“Hersi amekuwa akionekana na timu muda mwingi kuanzia mazoezini hadi wakati wa mazoezi, ila huoni hicho kikifanyika kwa viongozi wa Simba, ndio maana nasisitiza ukweli wa timu yao kutofanya vizuri upo kwao.”

Amesema Simba itasubili dakika 90 kujua kama msimu ujao itacheza Ligi ya Mabingwa ama Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), kitu ambacho hajaona kama kimekaa sawa kwa upande wao.

“Yanga na Simba zimekuwa vizuri Ligi ya Mabingwa zinapaswa kuwa na muendelezo, ila kwa hicho kinachoendelea Simba, isipozinduka Yanga inaweza ikachukua mataji ya Ligi Kuu hata mara saba na nimpongeze injinia amefanya mabadiliko makubwa kwenye mpira wa miguu na ni mfano wa kuigwa na wengi,” anasema.

VITA YA FEI NA AZIZ
Staa huyo anafurahishwa kuuona ubora wa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akidai kinachompa burudani zaidi ni bato la ufungaji wa mabao baina yake na Stephane Aziz Ki.

“Dakika 90 zitaamua nani anastahili kiatu cha dhahabu kati ya Fei Toto ambaye najivunia kumuona akifanya vizuri kama mzawa, pia Aziz Ki mfano mechi ya juzi hadi akafunga kwa kichwa jambo ambalo hajawahi kulifanya, ila anataka aache rekodi yake ya kusimuliwa,” amesema.

Related Posts