Na Grace Mwakalinga, Mtanzania Digital
SHIRIKA la Organization for Community Engagement (OCE), limeiomba Serikali kufanya tathmini ya athari za kimazingira zinazoweza kutokea kutokana na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi (EACOP) linalojengwa kuanzia Kabaale – Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani jijini Tanga -Tanzania.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Richard Senkondo, Mei 27,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu athari za mazingira kutokana na ujenzi wa bomba hilo la mafuta.
Amesema faida za kufanyika kwa tathmini za athari za mazingira katika ujenzi huo wa mafuta ni kuokoa maisha ya viumbe hai na mimea ambayo uwepo wake unasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema ujenzi wa bomba hilo ambalo linapitishwa chini ya ardhi linaweza kusababisha ongezeko la joto ambalo litasabisha madhara kwenye afya za binadamu na mimea.
“Tangu mradi huu unaanza sisi wadau wa mazingira tumekuwa tukiishauri serikali kuangalia kwa jicho la kipekee athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na bomba hilo, tumeona hasara ni kubwa kuliko faida hasa kwenye suala la mazingira hewa kubwa ya ukaa itazalishwa na ongezeko la joto litaongezeka jambo ambalo ni hatari kwa viumbe hai na mimea,” amesema Senkondo.
Amesema miongoni mwa hatua walizoanza kuchukua katika kuhakikisha jambo hilo linachukuliwa kwa umuhimu ni pamoja na kufika katika Ubalozi wa China nchini Tanzania ambao wamekuwa ni sehemu ya ufadhili katika mradi huo wa ujenzi wa bomba la mafuta kuwaomba kutambua athari za kimazingira.
Mtaalam wa mabadiliko ya tabianchi na nishati jadidifu, Baraka Machumu, amesema Tanzania itanufaika kwa asilimia 15 katika mradi huo na kwamba ili mradi huo ulete tija kwa watanzania yapaswa mafuta yachakatwe nchini kwa ajili ya kupata fedha zikazosaidia kukabiliana na athari za kimazingira kutokana na bomba hilo.
Amesema Tanzania itapitisha bomba la mafuta ghafi kuelekea mataifa yanayofadhili mradi huo huku miundombinu na makazi ya wananchi yakichukuliwa kwa fidia ya kiasi ambacho waliopisha mradi wanasema hakikidhi mahitaji ya sasa.
Miongoni mwa wavuvi kutoka jijini Tanga, Bausi Ramadhan amesema baada ya kupisha eneo kujenga bomba hilo kwa sasa wanatumia umbali mrefu kufuata samaki.
Amesema maisha yao yapo hatarini kwa sababu samaki hao wanapatikana umbali mrefu na hawana vifaa vya kisasa vya kuvulia.
Mradi wa Bomba la Mafuta ghafi la Afrika Mashariki (ECOP) una urefu wa kilomita 1,443 kati ya hizo 296 zipo nchini Uganda na 1147 zipo Tanzania na kupita mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
Lengo la mradi huo ni kuwezesha mafuta yatakayozalishwa nchini Uganda kusambazwa kwenye soko la ndani na sehemu inayobaki kuuzwa nje kwenye soko la kimataifa kupitia bomba la mafuta.