KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, ameweka wazi kilichomuumiza na kumkwamisha msimu huu katika kupambana kufikia malengo aliyojiwekea.
Muivory Coast huyo aliyejizolea umaarufu kwa mashabiki wa kikosi hicho ndani ya msimu mmoja aliotumika akitokea ASEC Mimosas, amesema pamoja na mafanikio, lakini alishindwa kucheza mechi muhimu hususan za kimataifa kutokana na majeraha.
“Majeraha ni jambo lililonikwamisha sana kwani nilishindwa kucheza mechi muhimu hasa za kimataifa. Kuna muda nilikuwa naona kabisa uwepo wangu unahitajika (kikosini) na sikuweza kucheza,” amesema mchezaji huyo.
“Sioni kama nimetumika hata nusu au robo ya kiwango changu. Lakini maumivu ambayo niliyapata msimu huu sitaki yajirudie tena wakati ujao.”
Katika msimu mmoja amecheza mechi 21 kati ya 29 ilizocheza Yanga, akiwa na mabao saba na asisti nne katika ligi, akiwazidi washambuliaji wa timu hiyo Kennedy Musonda mwenye matatu na Clement Mzize manne.
Pacome ameeleza kuwa licha ya furaha kubwa ya ubingwa, msimu huu kwake unabaki kuwa historia ya mambo yaliyompa wakati mgumu.
Ameongeza kuwa,”msimu wangu wa kwanza nimeufurahia na nimeona upendo mkubwa kwa mashabiki wakati wote nilipocheza hata nilipokuwa nje. Wameniongezea deni kubwa sana moyoni na nitawapa furaha zaidi msimu ujao.
“Ingawa hatujachukua Kombe la FA na tumeishia robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika hayo yote kwa upande wangu nayachukua kama deni na kwenda kuyalipa msimu ujao.”
Pacome alitolewa uwanjani kutokana na jeraha katika mechi dhidi ya Azam FC iliyopigwa Machi 17, mwaka huu, jambo lililosababisha kukaa nje na kukosa mechi za kimataifa dhidi Mamelod Sundowns ambako ndiko Yanga ilimalizia safari yake.