Moshi. Siku tatu baada ya kutokea kifo cha Ephagro Msele (43) anayedaiwa kuuawa kwa kuchomwa kisu na mkewe Beatrice Elias (36), Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewakabidhi ndugu mwili wa marehemu.
Kwa mujibu wa Polisi, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Mei 25, 2024 saa 3:50 usiku katika Kitongoji cha Pumuani A, Kata ya Kirua Vunjo, ambapo Msele ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Katanini, Kata ya Karanga aliuawa sababu zikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Mashuhuda wameeleza kuwa, tukio hilo lilitokea baada ya Beatrice kumfuatilia nyumbani kwa mwanamke mwingine aliyezaa naye na kugombana kabla ya kumchoma kisu.
Akizungumza na Mwananchi jana, kaka wa merehemu, Philip Msele amesema baada ya mwili wa ndugu yao kufanyiwa uchunguzi wanapanga taratibu za mazishi.
“Leo tumewenda KCMC kufanya postmortem na shughuli imefanyika, tunashukuru Jeshi la Polisi wametukabidhi mwili kwa ajili ya maandalizi ya maziko kwa ndugu yetu,” amesema.
Amesema baada ya kukabidhiwa mwili, watakuwa na kikao cha familia nyumbani kwa marehemu na kupanga siku ya maziko.
“Marehemu Epharo Msele atazikwa hapa nyumbani kwake Katanini, ameacha watoto saba, watoto sita ni wa mama hapa nyumbani na mwingine mmoja ni wa mwanamke mwingine,” amesema.
Kuhusu marehemu kuwa na mke mwingine, amesema; “Hajawahi kutushirikisha sisi kama familia kwamba ana mji mwingine, ila baada ya hili tukio sisi kama familia tulienda eneo la tukio kesho yake, na hata majirani walitueleza mji ule ni wa ndugu yetu.”
Akimzungumzia Msele, mmoja wa marafiki zake, Joachim Joseph, amesema alikuwa ni mtu mwenye upendo na kila mtu na kwamba licha ya kuwa ni baba ubatizo wa mwanaye, hakuwahi kumshirikisha jambo lolote gumu analopitia.
“Marehemu Msele alikuwa ni mtu wangu wa karibu sana, ni baba ubatizo wa mwanangu, nilipopata hizo taarifa nilishtuka sana kwa sababu yeye ni mtu wa dini na wa kanisani.
“Sikutazamia kama kuna kitu kama hiki ambacho kingeweza kumtokea, kwa kweli nilishtuka sana, maana ni jambo la kushangaza,” amesema.
Wakati waadishi wa Mwananchi wakiwa msibani Katatani, wameshuhuda watoto wa marehemu wakiwa na bashasha ya kwenda kumwona mama yao gerezani, walibebwa na gari la kifahari wakaondoka na babu yao, wakiwa hawafahamu watamkuta katika mazingira gani na muda mfupi baadaye walirudi wakiwa na majonzi.
Akizungumza na Mwananchi, babu yao ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema: “Sasa hivi hapa nataka nichukue watoto niwapeleka wakamwone mama yao, wengine wametoka shule walikokuwa wanataka kujua mama yao yuko wapi, maana hakuna baba hakuna mama, unafikiri ni kitu gani kinatokea,” amesema.
Mei 25, mwaka huu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi na kuwa mwanamke huyo alimvizia mume wake akitoka kwa mzazi mwenzake na kumchoma na kitu chenye ncha kali.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Pumuani A, Abrahaman Mnyanyemba, amesema jana Mei 26 kuwa alipofika eneo la tukio alikuta mwili wa mwanamume huyo ukiwa chini huku ukitokwa na damu nyingi.
Amesema polisi waliofika eneo la tukio walikagua mwili na kubaini mwanaume huyo alichomwa na kisu mgongoni na walipotafuta kisu kilichotumika walikikuta ndani ya pochi ya mwanamke huyo kikiwa kimefichwa pamoja na simu na pochi ya mwanaume.