MWAKA 2018 kuelekea msimu mpya wa 2018/19, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ilikuwa na mojawapo wa mawazo bora kuwahi kutokea kwenye mpira wa Tanzania.
Nalo ni wazo la kuanzisha mfumo wa mtoano (play off) ulioanzia kwenye Ligi Kuu pekee na baadaye kuhamia Ligi Daraja la Kwanza (Championship).
Hilo ni wazo zuri katika muktadha wowote kwa mtu mwenye kuutakia mema mpira wetu.
Ili mpira uendelee kabla ya mambo mengine yote, kwanza unatakiwa uchezwe. Kanuni au sheria yoyote inayosababisha mpira uchezwe zaidi na zaidi, hiyo ni kanuni au sheria yenye afya kwa mpira.
Mfumo huu wa mtoano unafanya mpira uchezwe yaani unaongeza mechi – unaongeza mashindano. Pata picha ligi zingekuwa zinaisha tu na waliopanda wamepanda na walioshuka wameshuka tunaishia hapo.
Hizi mechi za ‘play-offs’ zisingekuwepo maana yake mashindano yangepungua. Hiyo siyo afya ya mpira. Kwa hiyo hapa Bodi ya Ligi walicheza kama Pele kuleta mfumo huu.
Mpira unachezwa, watu wanapata raha, wanafurahi.
Mechi hizi za mtoano ni fursa kubwa sana ya biashara.
Zinatakiwa kutengenezewa utaratibu mzuri utakaoleta hela kwenye mpira kuanzia haki ya matangazo ya televisheni hadi udhamini wa pamoja na mmoja mmoja.
Kwa nchi zilizoanza siku nyingi kutumia mfumo huu kama England, mechi hizi ni kubwa sana. Fainali ya Leeds United na Southampton wikiendi hii ilitazamwa na watu wengi zaidi kuliko fainali ya Kombe la FA kati ya Manchester City na Manchestet United wikiendi hiyohiyo.
Hii ni kwa sababu mechi hizi huleta msisimko wa aina yake.
Msisimko huo ndiyo biashara.
Mechi hizo zinatengeneza muunganiko baina ya ligi zote zilizopo chini ya Bodi ya Ligi, Ligi Kuu, Championship League na First League.
Timu za Ligi Kuu hucheza mechi hizi na timu za Championship, na timu za Championship hucheza mechi hizi na timu za First League.
Maana yake mfumo huo umetengeneza muunganiko wa madaraja yote yaliyo chini ya Bodi ya Ligi ambayo ni madaraja ya kulipwa.
Kanuni za ligi zote tatu zilizo chini ya Bodi ya Ligi zinaeleza wazi kwamba timu mbili kutoka daraja la chini zitapanda moja kwa moja kwenda daraja la juu.
Lakini kanuni hizo zinatoa nafasi ya pili kwa timu za tatu na nne kwenye kila daraja kujaribu bahati kupitia mechi hizi. Hii huongeza ushindani kwenye ligi kwa sababu nafasi hizo pia zina thamani.
Ingekuwa tu kwamba wa kwanza na wa pili wanapanda, basi nafasi za tatu na nne zingekosa thamani kama ilivyo sasa.
Haya yote ni mambo mema na mazuri yanayoletwa na mfumo huu uliopo Tanzania.
Tanzania imekuwa mbele katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuja na mabadiliko chanya.
Mwaka 2006, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Leodeger Tenga, lilibadilisha mfumo wa msimu wa soka kutoka ule wa asili wa Januari – Desemba ambao ulikuwa ukifuata kalenda ya mwaka, hadi wa Agosti – Mei tunaotumia sasa.
Mfumo wa msimu mpya ambao ulianza 2007/08 ulilenga katika kufuata mifumo ya misimu ya dunia ambayo hutumiwa hadi na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Kwa kufanya hivyo, Tanzania ikawa nchi ya kwanza katika ukanda wa Cecafa.
Sasa hivi nchi nyingi za Cecafa zimehamia kwenye mfumo huo na sasa tunazungumza lugha moja.
Hakuna zuri lenye mazuri kwa asilimia mia moja. Lazima tu litakuwa na asilimia fulani za mabaya ili kuleta ukamilifu wa kibinadamu katika uanzishwaji wa jambo husika.
Likiwa zuri kwa asilimia mia moja, hilo halikuanzishwa na binadamu. Kwa hiyo hata huu mfumo wetu una upungufu kidogo. Wakosoaji wa mfumo wa mechi za mtoano (play-offs) wanasema zinaminya nafasi ya timu nyingine kusonga mbele.
Wao wangependa kuona timu za daraja moja zicheze zenyewe kwa zenyewe bila kukutana na timu za madaraja mengine, hasa ya juu. Wanasema hii inazoenea timu za madaraja ya chini. Kwao, huo ni mfumo tata.
Ni kweli, kuzikutanisha timu za madaraja tofauti katika mechi hizo ni kutoa nafasi ndogo kwa zile za madaraja ya chini kunufaika. Ingekuwa tu timu za daraja moja zikutane zenyewe kwa zenyewe kuamua kupanda au kushuka.
Hata hivyo, bado mfumo huo unaleta chachu ya mashindano — ndiyo utamu. Ni sawa tu na pilipili, kule kuwasha ndiyo raha yake.
Mbona kwenye mashindano mengine kama Kombe la Shirikisho (FA) hukutanisha timu za madaraja tofauti na zinacheza!