“Samia Skolashipu siyo mkopo, Serikali itakulipia gharama zote” Mkenda

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) leo (Jumatatu, Mei 27, 2024) amezindua miongozo ya utoaji wa ruzuku na mikopo kwa mwaka wa masomo 2024-2025 na kuwataka wanafunzi kusoma kwa juhudi ili kunufaika na fursa zinazotolewa na serikali kupitia mikopo na ruzuku.

Miongozo iliyozinduliwa ni ‘Mwongozo wa Utoaji Ruzuku za Samia kwa mwaka 2024-2025’; ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Shahada za Kwanza kwa 2024-2025’; ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Stashahada (Diploma) kwa 2024-2025’; ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Stashahada ya Umahiri katika Sheria kwa 2024-2025 (Post Graduate Diploma in Legal Practice)’.

Prof. Mkenda amezindua miongozo hiyo katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Popatlal, Jijini Tanga katika hafla ambayo pia aliitumia kuzindua maonesho ya ‘Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu’ – jukwaa linalojumuisha wadau wa elimu kuonyesha kazi za utafiti, ujuzi na kutoa elimu kwa umma kuhusu kazi mbalimbali za sekta ya elimu.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa wanafunzi kusoma kwa juhudi, Prof. Mkenda amewataka wanafunzi wanaosoma tahasusi za sayansi kusoma kwa bidii ili kupata ufadhili wa Samia Skolashipu ambao u nawalenga wanafunzi wa tahasusi za sayansi takribani 700 wenye ufaulu wa juu katika mitihani yao ya kidato cha sita.

“Samia Skolashipu siyo mkopo, Serikali itakulipia gharama zote za kujikimu, ada, gharama za mabweni, vifaa vya kusomea … ili mradi uwe unasoma shahada za sayansi, sayansi ya tiba, TEHAMA, hisabati na uendelee kufanya vizuri katika vyuo vikuu,” amesema Prof. Mkenda.

Akizungumza pembeni mwa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia amesema kuwa miongozo iliyozinduliwa itapatikana katika tovuti za HESLB na Wizara ya Elimu (www.heslb.go.tz na www.moe.go.tz ) kuanzia kesho (Jumanne, Mei 28, 2024) ili wanafunzi wasome kabla ya dirisha la maombi kwa njia ya mtandao kufunguliwa.

“Dirisha la uombaji mikopo litafunguliwa kwa siku 90 kuanzia Juni 1 – Agosti 30, 2024 ili kuwapa waombaji mikopo muda wa kutosha,” amesema Dkt. Kiwia.

Related Posts