Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ametoa agizo kwa mameneja wa mikoa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha wanatoa taarifa za barabara zinazohitaji matengenezo haraka ili kuepusha ujenzi upya usio wa lazima.
Akizungumza leo Jumatatu, Mei 27, 2024, wakati akifungua maonyesho ya sekta ya ujenzi katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Dk Tulia ameweka bayana umuhimu wa hatua za haraka katika kuimarisha ubora wa barabara.
Maonyesho haya ya siku mbili yameandaliwa na Wizara ya Ujenzi na taasisi zake, yakilenga kutoa elimu na huduma kuhusu kazi wanazofanya, huku yakidhamiria kuonyesha mageuzi makubwa yaliyofanywa katika sekta ya ujenzi. Akieleza matumaini yake, Dk Tulia amesema kuwa Wizara ya Ujenzi imepokea magari mapya ya kupima ubora wa barabara, hatua itakayosaidia kuepusha matatizo ya zamani ya barabara kuharibika punde tu baada ya ujenzi.
“Barabara mpya zinaanza kuonyesha mashimo mara tu mvua inaponyesha, jambo linalosababisha gharama za ziada kwa Serikali. Tunapaswa kuepusha hali hii kwa kuhakikisha ubora wa barabara tunapozipokea,” amesema Dk Tulia, akitoa mfano wa barabara ya Dodoma – Iringa iliyohitaji kujengwa upya licha ya kuwa mpya.
Akizungumzia vifaa vipya vilivyopokewa na Wizara ya Ujenzi, Dk Tulia amesisitiza umuhimu wa vifaa hivyo kutumika ipasavyo. “Vifaa hivyo vikafanye kazi ambayo imekusudiwa,” ameongeza.
Dk Tulia pia ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) kwa kuanzisha huduma za kumfuata mteja alipo, hatua inayorahisisha huduma kwa wananchi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mabadiliko haya yanapaswa kuendana na utoaji bora wa huduma ili kuepusha malalamiko ya awali kuhusu utendaji wa wakala huo.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akimkaribisha Spika Tulia, amebainisha mageuzi makubwa ndani ya wizara hiyo yanayotokana na uwezeshwaji mkubwa wanaoupata.
Amesema wamejipanga kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi ili kutimiza malengo ya kiongozi mkuu wa nchi katika sekta ya ujenzi.
Maonyesho haya ya siku mbili yatahitimishwa na uwasilishaji wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2024/25, hatua inayotarajiwa kuonyesha mipango mikubwa ya maendeleo katika sekta hiyo muhimu.