UHUSIANO Baina ya Tanzania na Ufaransa umeendelea kuimarika hususani katika masuala ya biashara na uwekezaji ambapo kampuni zipatazo 27 kutoka nchini Ufaransa zimewasili nchini na kukutana na wafanyabiashara wa Tanzania na kujadili namna ya kufanya biashara na uwekezaji utakaonufaisha mataifa hayo mawili kwa kuangazia masuala ya muindombinu na usafirishaji, nishati, ukuaji wa miji na sekta ya maji.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliowatanisha wafanyabiashara kutoka Ufaransa na Tanzania Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema, Mkutano huo ni mwendelezo wa mkutano uliofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei, 2022 nchini Ufaransa.
“Katika mkutano huo moja ya maelekezo ilikuwa ni kuhakikisha wafanyabiashara wa Ufaransa wanashirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa katika maeneo ya kuongeza thamani mazao ya kilimo kwa kuanza kukiboresha kilimo chenyewe na kukipa thamani kupitia uchakataji katika viwanda.” Amesema.
Kigahe amesema, Mkutano huo umelenga kuboresha zaidi na kampuni zaidi ya 27 zimeshiriki mkutano huo huku biashara baina ya Nchi hizo unakua ambapo Tanzania huagiza bidhaa kutoka Ufaransa kati ya dola milioni 75 kwa mwaka na Ufaransa huuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 25 kwa Tanzania na kuwataka watanzania kutumia fursa hiyo kwa kuuza bidhaa na kufanya biashara zaidi na Ufaransa.
Pia amesema kuwa mkutano huo utaongeza wigo zaidi kutokana na Ufaransa kuiangalia Tanzania kwa jicho pana katika uwekezaji kutokana na uwepo wa sera zinazovutia uwekezaji, utulivu wa kisiasa pamoja na miundombinu rafiki.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui amesema kuwa, uhusiano baina ya nchi hizo mbili umefikia katika ngazi ya juu na hiyo ni kutokana na uthubutu wa viongozi wa mataifa hayo mawili.
Amesema, Tanzania licha ya kuwa na Rais mwanamapinduzi katika masuala ya kiuchumi pia ina fursa nyingi za uwekezaji, sera madhubuti, utulivu pamoja na maeneo ya uwekezaji na kueleza kuwa kipitia mkutano huo watajenga uchumi mkubwa utakaonufaisha mataifa hayo mawili.
Pia Balozi wa Jumuiya ya Ulaya (EU,) nchini Tanzania Bi. Christine Grau ameeleza kuwa mkutano huo utaleta matokeo chanya kutokana na utulivu uliopo katika Nchi hizo na kusema kuwa Tanzania ni salama na himilivu katika uwekezaji, ina mazingira wezeshi, nguvu kazi toshelevu hususani vijana pamoja na utulivu wa kisiasa na amani.
Awali Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Ali Mwadini alieleza kuwa mkutano huo utaweka daraja imara baina ya sekta binafsi ambazo huchangia uchumi kwa kiasi kikubwa duniani kote na hiyo ni pamoja na kubadilishana uzoefu katika teknolojia.
“Tanzania ipo vizuri, Tuna rasilimali, sera pamoja na soko la uhakika kupitia usafiri wa anga pamoja na reli ya kisasa inayounganisha Nchi za jirani na utulivu wa kisiasa, amani na upekee wa sekta ya utalii vimekuwa tunu kubwa inayowavutia wawekezaji.” Amesema.
Mkutano huo utafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na siku moja Visiwani Zanzibar utajadili masuala ya uwekezaji na biashara kwa kuhusisha masuala ya miundombinu, nishati, matumizi ya gesi na ukuaji wa miji.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe akizungumza wakati wa mkutano huo na kuwataka watanzania kutumia fursa za kibiashara kutoka Ufaransa hususani katika masuala ya teknolojia, nishati na gesi. Leo jijini Dar es Salaam.
Zoezi la utiaji saini hati ya makubaliano ya utunzaji wa mazingira likiendelea.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.