Dar es Salaam. Magonjwa kama homa ya mapafu na mengine yanayohusiana na baridi, yanatarajiwa kuwakabili wananchi katika kipindi cha kuanzia Juni hadi Agosti 2024.
Uwezekano wa kutokea kwa magonjwa hayo, unatokana na matarajio ya kuanza kwa msimu wa kipupwe, utakaosababisha hali ya baridi ya wastani na joto kiasi.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), katika kipindi hicho kunatarajiwa pia kuwepo na vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo na hivyo kuibua magonjwa ya macho.
Hizo ni baadhi ya tahadhari zilizotolewa leo Jumatatu Mei 27, 2024 na TMA ikitazungumzia matokeo ya msimu wa kipupwe utakaoanza Juni.
Sambamba na tahadhari hizo, nyingine zilizotolewa na mamlaka hiyo ni uwezekano wa kutokea magonjwa ya mifugo na macho kutokana na vumbi.
“Tunatoa tahadhari za kiafya zichukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi hilo,” imeeleza taarifa hiyo.
Kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi kwa kipindi hicho, TMA inapendekeza maji na malisho vitumike kwa uangalifu ili kupunguza athari inayotarajiwa kujitokeza.
“Wakulima wanashauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo yenye unyevu na maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hicho,” amesema.
Katika kipindi hicho, mikoa ya kusini mwa Morogoro, Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe inatarajiwa kuwa na baridi ya wastani hadi kali.
“Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza Julai ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7 na 15 na katika maeneo yenye miinuko kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7,” imesema TMA.
Kwa mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu, itapata baridi ya wastani na joto kati ya nyuzi joto 15 na 20.
Kwa upande wa Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba, hali ya joto kitakuwa kati ya nyuzi joto 23 na 26.
Lakini maeneo ya mwambao wa Pwani na visiwani hali itakuwa kati ya nyuzi joto 17 na 23, huku maeneo yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 17.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kilimanjaro, Arusha na Manyara inatarajiwa na nyuzi joto 15 na 20.
Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma na kwamba joto la chini kwa mujibu wa TMA, litakuwa kati ya nyuzi joto 15 na 20.
Kanda ya Kati mikoa ya Singida na Dodoma hali itakuwa kati ya nyuzi joto 11 na 17.
TMA imesema ukanda wa Pwani ya Kusini inayohusisha Mikoa ya Mtwara na Lindi hali itafikia nyuzi joto 17 na 22.
Mkoa wa Ruvuma hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 na 18.