Mbeya/Dar. Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, hatima ya uchaguzi uliofutwa wa kumpata mwenyekiti mpya wa Mkoa wa Njombe bado iko gizani.
Uchaguzi wa kanda hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 29, 2024 katika mji wa Makambako mkoani Njombe, unawakutanisha wabunge wa zamani, Joseph Mbilinyi (Sugu), Peter Msigwa na utashirikisha wapiga kura 120 kutoka mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa.
Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, miongoni mwa wajumbe wanaopiga kura katika uchaguzi wa kanda ni pamoja na mwenyekiti wa mkoa ambaye kwa Njombe hadi keshokutwa Mei 19, 2024 atakuwa hajapatikana.
Hata hivyo, akizungumza leo Mei 27, 2024 Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chadema, Benson Kigaila amesema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, uchaguzi wa juu ngazi ya chama hicho huwa unafanyika baada ya ngazi ya chini kukamilisha walau kwa asilimia 50.
“Ngazi za chini kwa Kanda ya Nyasa ni mikoa ambayo ipo mitano, mingine yote imefanya uchaguzi kasoro Njombe, ambayo katika wilaya zake zote wameshafanya uchaguzi na zitashiriki.
“Ni viongozi wa mkoa tu hawatashiriki na wasiposhiriki hao hata kama ungekuwa mkoa mzima akidi ya uchaguzi ingekuwa imetimia kwa asilimia 80, ambayo ni zaidi ya silimia 50 inayotakiwa na Katiba,” amesema.
Kigaila amesema hadi sasa maandalizi ya uchaguzi wa kanda hiyo yamekamilika na hakuna taarifa waliyopokea ya kuweka tahadhari.
Amesema Mei 29 utafanyika uchaguzi katika kanda tatu kati ya nne – Nyasa, Magharibi na Serengeti na kwamba ofisi ya Katibu Mkuu inaamini wagombea wanafuata misingi ya kampeni.
“Sijajua kwa nini Nyasa ndio inafuatiliwa zaidi ilhali Jumatano tutafanya uchaguzi kanda tatu, lakini niseme tunaridhishwa na mchakato ulivyo na maadalizi yanaendelea vizuri,” amesema.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo, Mchungaji Msigwa anayetetea nafasi yake amesema kampeni zao si za majukwaani bali mikakati ni mingi na anahitaji kuwa kwenye utulivu.
“Mengi tumezungumza, kwa sasa nahitaji kuwa kwenye utulivu na ukizingatia kampeni zetu si za majukwaani, mikakati ni mingi na leo sina cha nyongeza nasubiri siku ya uchaguzi,” amesema Msigwa.
Kwa upande wake Sugu amesema ameitikia wito wa mabadiliko, hivyo matarajio yake ni ushindi ambao hautakuwa wa kwake bali wa chama kwa ujumla.
Amesema iwapo atafanikiwa kushinda atatetekeleza vipaumbele vyake 10 akianza na ujenzi wa ofisi za chama hicho katika kanda na kwamba hatachangisha wanachama kabla ya kuweka mchango wake.
“Kwa sasa nipo najiandaa kwenda Njombe, nina vipaumbele 10 ikiwamo ujenzi wa ofisi ya kanda na kurudisha chama kwa wanachama, lakini ushindi hautakuwa wangu bali wa chama, mimi nimeitikia wito wa mabadiliko,” amesema Sugu.
Mchambuzi wa siasa jijini Mbeya, Prince Mwaihojo anasema mtifuano wa wawili hao Sugu na Msigwa unaakisi kukua kwa chama, lakini umaarufu wa wagombea hao.
Anasema pamoja na upinzani uliopo, atakayeshinda au kushindwa atakuwa ameonyesha ukomavu, japokuwa inaweza kumuathiri atakayeshindwa, haswa kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.
“Wale wote ni wagombea 2025 kwenye majimbo yao, hivyo atakayeshindwa anaweza kuathirika kwenye uchaguzi mkuu, lakini kwa ujumla wote wana nguvu kubwa nje na ndani ya chama,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kigaila amesema hatima ya kurejea uchaguzi wa Mkoa wa Njombe uliohairishwa baada ya kuzuka vurugu, itajulikana baada ya chama kufanya kikao na kutoa ratiba mpya.
Uchaguzi wa awali ambao awali Rose Mayemba alitetea kiti chake, ulitenguliwa Mei 24, 2024 baada ya mpinzani wake Ahadi Tweve na baadhi ya wajumbe kudai kuwa wajumbe kutoka Wilaya ya Makate hawakuwa halali.
Walikuwa wanadai kuwa viongozi wengi katika wilaya hiyo wanakaimu nafasi hizo kwa muda mrefu na kwamba hawakustahili au kuwa na sifa za kupiga kura kuchagua viongozi wa mkoa huo, hivyo wakashinikiza uahairishwe.
Kigaila amesema baada ya kuahirishwa uchaguzi huo utafanyika siku itakayotangazwa na chama.
Kigaila amesema baada ya kukaa vikao hivyo watatangaza mbele ya umma.
Hata hivyo, Kigaila amefafanua sintofahamu iliyozuka na kuahirishwa uchaguzi huo kuwa ni kutokuelewa kwa baadhi ya wapiga kura kwa nini viongozi wa muda wapige kura.
“Kwa kuzingatia Katiba yetu kiongozi yeyote anayekaimu nafasi au kuwekwa kwa muda kutekeleza majukumu fulani kwa muda fulani anakuwa na sifa au hadhi ya kupiga kura kama kiongozi mwingine, hivyo ndivyo ilivyo katika Katiba yetu,” amesema.