MARA paap! Ligi imeisha. Timu zote 16 ziko viwanjani leo kuanzia saa 10:00 jioni huku asilimia kubwa zikiombeana dua mbaya. Lakini kuna bato nne za kuvutia zinazosubiriwa kwa hamu.
Yanga tayari imeshatangazwa mabingwa baada ya kuutetea kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kwa ujumla huku Mtibwa Sugar ikishuka daraja. Walima miwa walichapwa mabao 3-2 na Mashujaa. Wana pointi 21 ambazo zimewashusha daraja moja kwa moja.
Mwanaspoti linakuletea bato nne kali ambazo zinatarajiwa kuamuliwa katika mechi nane za leo katika kuhitimisha msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Huenda hii ndio vita yenye mvuto zaidi inayosubiriwa kati ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC na Stephane Aziz Ki wa Yanga ambao wote hadi sasa wanawania Tuzo ya Ufungaji Bora kutokana na kila mmoja wao hadi sasa kufunga mabao 18.
Yanga inakamilisha ratiba dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex lakini akili zao zote ni kwa Aziz kuhakikisha anatwaa Kiatu cha Dhahabu Dar es Salaam. Lakini Azam FC ikiwa ugenini kucheza na Geita Gold nayo ina vita ya kuwania nafasi sambamba na kiatu cha Fei.
Katika mabao yake 18, Aziz Ki amefunga matatu kwa penalti huku Fei Toto akiwa ana bao moja tu la penalti, jambo linaloweza kumpa faida zaidi ikiwa watalingana idadi ya mabao baada ya mechi za mwisho leo kutokana na kanuni za Ligi Kuu Bara msimu huu kwenye vita ya ufungaji bora ilivyo.
Iko hivi, kanuni ya (13:1) kuhusu mshindi wa Tuzo ya Mfungaji Bora inaeleza, ikiwa wachezaji zaidi ya mmoja wamefungana idadi ya mabao njia ya kwanza itakayotumika wataangalia mabao yaliyofungwa kwa njia ya kawaida yatapewa alama mbili (2).
Mabao yatakayofungwa kwa njia ya penalti yatapewa alama moja (1) na ikiwa watalingana pia itatumika kanuni ya (13:2) inayoelezea mchezaji aliyecheza dakika chache atakuwa mshindi na ikitokea wakalingana pia itaangaliwa kanuni ya (13:3).
Kanuni hiyo ya (13:3) inaeleza, kama vigezo vyote vilivyowekwa vinafanana pia basi, nyota aliyefunga mabao mengi ugenini atakuwa mshindi.
Ieleweke wazi kwamba, mpaka sasa takwimu zinaonyesha kuwa Fei Toto amecheza mechi 28 kwa dakika 2,352, wakati Aziz Ki akiwa na dakika 1,994 katika mechi 25.
Mbali na kutaka kuibuka tu kidedea ila kila mchezaji anaweza kujitengeneza rekodi yake kwani endapo Feisal atafunga bao angalau moja tu ataifikia rekodi ya mabao 19 iliyowekwa na aliyekuwa nyota wa Azam FC, John Bocco msimu wa 2011/2012 ya kuwa mchezaji wa timu hiyo aliyefunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu.
Kwa upande wa Aziz Ki licha ya kuwania tuzo hiyo ila wengi wanaangalia ni vipi anaweza kuifikia au kuivunja rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Amissi Tambwe aliyefunga mabao 21 ndani ya msimu mmoja aliyoiweka 2015/2016.
Miamba hii inawania nafasi moja ya timu ambayo itaungana na Yanga kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao.
Timu zote hadi sasa zina pointi 66 ila Azam FC inanufaika na utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa jambo linaloongeza utamu wa kutaka kujua mmoja kati yao nani atakayeungana na Yanga huku mwingine akiungana na Coastal Union kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikaribisha JKT Tanzania na ikiwa itashinda itaiombea mabaya Azam ambayo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Geita Gold inayopambania kutoshuka daraja, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita. Katika mechi mbili ambazo Azam imecheza na Geita ugenini haijashinda zaidi ya kuambulia sare pekee.
Katika msimamo, Azam imeizidi Simba kwa tofauti ya mabao manane na ikiwa timu zote zitashinda basi matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam watafuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao huku kwa upande wa kikosi hicho cha Msimbazi kikienda Kombe la Shirikisho.
Wakati Simba ikihitaji ushindi hali hiyo ni sawa na wapinzani wao, JKT Tanzania iliyopo nafasi ya 12 na pointi zake 32 kwani haipo salama hadi sasa na inapigania kuepuka katika janga la kucheza michezo ya mtoano (Play-Offs) ili kubaki msimu ujao.
Leo itapatikana timu moja kati ya Geita Gold au Tabora United itakayoungana na Mtibwa Sugar kucheza Ligi ya Championship msimu ujao.
Mtibwa ambayo ni mabingwa wa zamani wa Tanzania msimu wa 1999 na 2000, tayari imeshatangulia mapema tu ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka 28 tangu timu hiyo ilipoanzishwa mwaka 1988 na kupanda Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) 1996.
Timu hiyo imeshuka baada ya kukusanya pointi 21 ambapo hata leo ikiifunga Ihefu haitoweza kujiokoa zaidi ya kukamilisha tu ratiba.
Geita Gold iko nafasi ya 15 na pointi 25 na leo itacheza dhidi ya Azam huku Tabora United inayoshika nafasi ya 14 na pointi 27 itakuwa na kibarua kigumu ugenini dhidi ya Namungo, mechi ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa huko Ruangwa mkoani Lindi.
Ikiwa timu hizo mbili zitashinda michezo yao ya mwisho basi ni wazi Geita itashuka rasmi daraja huku Tabora United ikiangukia katika nafasi ya ‘Play-Offs’ ambayo itazikutanisha miamba iliyomaliza nafasi ya 13 na 14 ili kujitetea tena kubaki msimu ujao.
Maombi ya Geita ni kuomba iifunge Azam FC na kufikisha pointi 28 huku ikiiombea Tabora United ifungwe ili iangukie michezo ya mtoano.
Namungo inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kujihakikishia kubaki salama kwani pointi 33 ilizonazo ni sambamba na za Singida Fountain Gate, Dodoma Jiji na Ihefu huku Mashujaa iliyopo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 32 sawa na JKT Tanzania.
Bato nyingine ni hii ya kugombania kuwa Kipa Bora wa msimu huu ambapo hadi sasa Djigui Diarra wa Yanga na Ley Matampi wa Coastal Union ndio wanaochuana katika tuzo ya Glovu za Dhahabu kutokana na wote kufikisha ‘Clean Sheets’ 14 katika Ligi Kuu Bara msimu huu. Wote ni raia wa kigeni.
Diarra anaipambania tuzo hii kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuchukua misimu miwili iliyopita lakini kwa Matampi huu ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union akitokea Klabu ya Jeunesse Sportive Groupe Bazano ya kwao DR Congo.
Makipa wote wawili wamekuwa na mchango mkubwa ndani ya timu zao hadi sasa ambapo Diarra ameiwezesha Yanga kutetea taji lake la ligi huku kwa upande wa Matampi akiiwezesha Coastal Union kumaliza nafasi ya nne na kufuzu michuano ya kimataifa msimu ujao.
Coastal imepata nafasi hiyo baada ya kufikisha jumla ya pointi 42 ambazo haziwezi kufikiwa na timu zilizopo chini yake na kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1989 iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika na kuishia raundi ya kwanza.
Baada ya hapo ndipo michuano hiyo ilikuja kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004.
Vita ya Matampi na Diarra inaangaliwa zaidi ili kujua ni nani kati yao ataibuka kidedea kutokana na msimu bora waliokuwa nao.
Yanga inacheza na Tanzania Prisons ambayo haina presha yoyote kwani imeshajihakikishia kubaki msimu ujao sawa na mchezo wa Coastal Union dhidi ya KMC ambao timu zote zinakamilisha ratiba hivyo ni mechi ya kusaka heshima tu baina yao.
Eneo jingine litakalohitimishwa leo ni kujua mbabe wa kutengeneza mabao yaani ‘asisti’ msimu huu ambapo hadi sasa nyota wa Azam FC, Kipre Junior ndiye anayeongoza akiwa nazo tisa akifuatiwa na Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyetengeneza nane.
Wengine wanaofuatia ni Yao Kouassi wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Lusajo Mwaikenda wote wa Azam FC waliotengeneza saba huku Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Clatous Chama (Simba) na Clement Mzize (Yanga) wakiwa nazo sita kila mmoja wao. Vita hii inaweza isiwe na msisimko mkubwa sana kwa kuwa haina tuzo yoyote.
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Denis Kitambi alisema jambo kubwa ambalo amewasisitiza wachezaji wa kikosi hicho ni kucheza kwa tahadhari kuanzia namna bora ya kujilinda na wakati huohuo wakishambulia kwa kuwashtukiza wapinzani wao.
“Tuko katika kipindi kigumu ila nimekaa na wachezaji na kuwataka kutocheza kwa kuangalia wengine na badala yake sisi jukumu letu ni kuhakikisha tunapata matokeo chanya na mwishoni ndipo tutakapojua hatma yetu kwa msimu ujao,” alisema Kitambi.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Tabora United, Masoud Djuma aliweka wazi itakuwa jambo la kushangaza kwake ikiwa timu hiyo iliyopanda daraja msimu uliopita itarudi tena kucheza Ligi ya Championship msimu ujao huku ikiwa chini ya mikono yake.
Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm anaamini kuwa Stephane Aziz KI anaweza kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara hata kama atakosa tuzo ya mfungaji bora ambayo anawania na Feisal Salum.
“Wote kwangu ni wachezaji wazuri na ubora wao ni mkubwa sana lakini nadhani Aziz anaweza kuwa mchezaji bora wa ligi kutokana na kuisaidia kwake Yanga kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu, kwangu yeyote kuwa mfungaji bora ni sawa, siwezi kubashiri kati yao,” alisema kocha huyo.
Kocha wa timu za vijana za Azam FC, Mohammed Badru amemtaja Feisal Salum kuwa anaweza kumzidi kete Aziz Ki kutokana na majukumu ambayo amekuwa kibebeshwa na timu hiyo.
“Feisal amekuwa akilitazama goli kwa karibu zaidi kuliko Aziz, Yanga wanaye mshambuliaji wa mwisho kiasili tofauti na Azam hivyo namuona Fei akifunga katika mchezo wa mwisho wa msimu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar.