Wameutumia mkutano huo kufikia makubaliano ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kufufua mazungumzo ya kuhusu biashara huria.
Mkutano huu umewaleta pamoja Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, Waziri Mkuu wa China Li Qiang na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida mjini Seoul kwa mazungumzo ya kwanza ya nchi hizo tatu baada ya karibu miaka mitano. Hapakuandaliwa mazungumzo yoyote katika kipindi hicho kutokana na janga la Uviko na pia kuzorota kwa uhusiano kati yao.
Korea Kaskazini ambayo haikuwa kwenye ajenda rasmi ya mkutano huo, saa chache kabla ya viongozi hao kukutana ilitangaza kwamba hivi karibuni itaweka satelaiti nyingine ya kijasusi kwenye anga, hatua ambayo inakiuka safu za vikwazo vya Umoja wa Mataifa vinavyoizuia kufanya majaribio kwa kutumia teknolojia ya masafa marefu. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Yoon na Kishida waliitaka Pyongyang kusitisha uzinduzi huo, huku kiongozi wa Korea Kusini akisema “utadhoofisha amani na utulivu wa kikanda na kimataifa”.
Maslahi ya pamoja
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo, nchi hizo zilisisitiza ahadi yao ya kuondoa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea, na kwamba amani inatumikia maslahi ya pamoja na ni jukumu la pamoja.
Waziri Mkuu Li alisema “China, Japan na Korea Kusini zinapaswa kushughulikia ipasavyo masuala nyeti na tofauti, kutilia maanani maslahi ya msingi ya kila mmoja na mashaka ya kila upande, kutekeleza kwa dhati dhana ya kufanya kazi kwa pamoja, kudumisha usalama na utulivu Kaskazini-mashariki mwa Asia, na kuhimiza amani ya kikanda na duniani.”
Soma pia: Korea Kusini na China zaahidi kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na usalama
China ikiwa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo awali ililaani majaribio ya nyuklia ya Korea Kaskazini na kuunga mkono vikwazo vinavyolenga kuzuia utengenezaji wa silaha zake.
Korea Kusini haina silaha za nyuklia, lakini inalindwa chini ya mwavuli wa nyuklia wa Marekani, ambayo imepeleka manowari zenye silaha za nyuklia katika luteka za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini.
Beijing imekuwa ikokosoa mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini, ikisema kwamba yanazidisha mivutano ya kikanda.
Soma pia:China yahimiza uhusiano thabiti na Korea Kusini licha ya “msuguano”
Katika mkutano huu nchi hizo tatu zimetangaza kwamba zitapanga majadiliano kwa ajili ya kuharakisha mazungumzo ya Nchi Tatu na kuimarisha ushirikiano ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya kilele mara kwa mara.
Taarifa hiyo pia ilijumuisha wito wa ushirikiano juu ya maendeleo uendelevu, huduma za afya, sayansi na teknolojia, na usimamizi wa majanga.