Vivuko Kigamboni, zigo zito kwa Temesa-2

Dar/Mikoani. Kama umewahi kuhisi maumivu ya kutwishwa mzigo mzito zaidi ya nguvu zako, basi hali hiyo ndiyo inayoukabili Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), katika jukumu la uendeshaji wa vivuko nchini.

Temesa inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwake ya mwaka 2005, inayotaka pamoja na majukumu mengine ya msingi, wakala huo uwajibike na uendeshaji wa uhakika na usalama wa vivuko nchini.

Jukumu hilo la kisheria badala ya kuwa fursa ya mapato kutokana na makusanyo ya vivuko, limegeuka shubiri na mzigo mzito kwa Temesa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi kwa takriban miezi mitatu umebaini hilo.

Uchunguzi umefanyika kutokana na malalamiko ya wananchi wanaotumia vivuko hivyo, ambao mara kadhaa wameeleza kutoridhishwa na huduma inayotolewa.

Hoja kubwa ya watumiaji wa vivuko waliozungumza na Mwananchi ni kuchelewa kwa huduma wanapofika eneo la kuvuka, kuharibika mara kwa mara kwa vivuko na hata uchache wake, kama inavyoelezwa na Salma Ally, mkazi wa Kigamboni.

Salma mfanyabiashara ya samaki Kibugumo, wilayani Kigamboni anasema inamchukua takribani saa moja kusubiri kuvuka Kigamboni-Magogoni.

Hilo ni tofauti na matarajio yake ya kutumia dakika 20 hadi 30 kuvuka eneo hilo kwenda lilipo Soko la samaki Feri.

“Ukitaka kufuata samaki ujue ukishafika hapa kwenye jengo la abiria utapoteza saa au zaidi kusubiri kivuko,” anasema Salma.

Kauli ya Salma inashabihiana na ya Abudi Abedi, mchuuzi wa samaki, anayesema analazimika kuamka alfajiri kuwahi sokoni.

“Natoka saa 10.00 alfajiri nyumbani Cheka, Kigamboni lakini nafika sokoni saa 12.00 asubuhi na wakati mwingine saa moja asubuhi. Panaponichelewesha ni eneo la kuvuka,” anasema.

Hali duni ya vivuko imewahi kuzua hofu kwa Mauwa Mussa, mkazi wa Kigamboni, baada ya kivuko kuzima katikati ya maji akiwa ndani yake.

“Sitaki kukumbuka ilivyokuwa, kila mmoja alifanya sala kwa imani yake. Nilikata tamaa kwamba nisingeweza kupona kwa sababu hata kutumia maboya siwezi,” anasema.

Mauwa anasimulia kivuko kilipovutwa na watu kushuka, hakuwa na fahamu na hata mizigo aliyokuwa nayo haikuwapo.

“Waliniibia mizigo yote baada ya kupoteza fahamu, nikapata hasara, wasiwasi na hadi sasa napanda kivuko roho ikiwa mkononi, siviamini,” anasema Mauwa.

Kwa Mauwa hali ikiwa hivyo, Asajile Michael anasema amekoma kutumia vivuko kuvuka yeye na kuvusha gari, badala yake anazunguka kupitia Daraja la Mwalimu Julius Nyerere.

Asajile anasema kivuko kilipopata hitilafu kikiwa katikati ya maji, akiwa na gari alihisi kiama.

“Nafanya kazi Posta, naishi Kigamboni Machava, nalazimika kuzunguka njia ya darajani, baada ya madhila ya kivuko, sirudii kupanda. Nimeizuia hata familia yangu,” anasema.

Mwananchi imebaini changamoto zinazosababisha kudorora kwa huduma zinachangiwa na uwezo mdogo wa Temesa kuendesha vivuko hivyo.

Hali hiyo inasababishwa na mapato yanayotokana na makusanyo ya nauli za abiria kutokutosheleza gharama za uendeshaji na haina ruzuku yoyote.

Mmoja wa maofisa waandamizi ndani ya Temesa (jina limehifadhiwa), anasema wakala huo unafanya shughuli zake kwa kujitegemea, haupokei ruzuku kutoka serikalini.

Mazingira hayo anasema yanafanya uendeshaji wa shughuli za wakala, vikiwemo vivuko uwe mzigo mzito.

Hata hivyo, ofisa huyo anasema kinachotoka Serikali Kuu, ni fedha za matengenezo makubwa, mishahara ya wafanyakazi wa kudumu na za utekelezaji wa miradi mikubwa.

Anasema matengenezo kinga, ukarabati wa vivuko, gharama za uendeshaji, mishahara ya wafanyakazi wa mkataba ambao ni asilimia 80 ya watumishi wote, vyote hivyo ni jukumu la Temesa.

Uchunguzi umebaini kati ya vivuko vyote 32 vinavyoendeshwa na Temesa nchini, asilimia 95 vinaendeshwa kwa mapato ya vivuko vya Kigamboni-Magogoni.

Hii ina maana mapato ya baadhi ya vivuko nje ya Dar es Salaam, hayatoshelezi hata kujinunulia mafuta ya dizeli kwa ajili ya kujiendesha.

Fedha za uendeshaji wa vivuko hivyo, hasa vya Pangani, Lindi na Mtwara zinatoka katika mapato ya vya Kigamboni-Magogoni, kwa mujibu wa nyaraka ambazo Mwananchi limeziona.

Hali hiyo kwa mujibu wa ofisa huyo wa Temesa, inavibebesha mzigo vivuko vya Kigamboni-Magogoni ilhali vyenyewe havina uwezo wa kujibeba.

Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kilahala akizungumzia hilo, amesema jukumu la wakala ni kuhudumia wananchi si kufanya biashara.

Kwa sababu ya jukumu hilo, anasema juhudi zinafanyika kuhakikisha huduma zinaendelea kuwafikia wananchi na kwa ubora uliokusudiwa.

“Sisi jukumu letu ni kuhudumia wananchi siyo kufanya biashara, ndiyo maana kama kuna eneo lina mapato machache tunalazimika (mapato) ya huku kupeleka kule, ilimradi wananchi waendelee kuhudumiwa, ndiyo dhamira ya Serikali,” anasema.

Kuhusu vivuko vinavyojiendesha bila kupata faida, Kilahala anasema inatokana na eneo husika na idadi ya abiria.

Anaeleza baadhi ya vivuko vipo katika maeneo yenye abiria wachache, hivyo makusanyo hutokana na idadi hiyo ndogo na kwa sababu wana haki ya kupata huduma, Serikali haina budi kuwahudumia.

Nauli hazikidhi uendeshaji

Mara ya mwisho nauli za vivuko zilipandishwa mwaka 2012, wakati huo hayati John Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi.

Wakati huo, nauli ilipanda kutoka Sh100 hadi Sh200 ambayo imedumu kwa miaka 12 bila mabadiliko yoyote.

Ingawa kutoongezeka kwake ni faraja kwa wananchi, uchunguzi umebaini kuwa kwa Temesa ni mzigo mwingine kutokana na ukweli kwamba, gharama za uendeshaji zimeongezeka.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, ofisa mmoja wa Temesa amesema nauli imebaki Sh200 ilhali bei ya mafuta, vilainishi na vipuli imeongezeka maradufu.

Mazingira hayo, anasema yanafanya gharama za uendeshaji ziwe zaidi ya kinachokusanywa, hivyo kusababisha baadhi ya mambo ya msingi yashindwe kufanyika.

“Unachokipata hakitoshi kugharimia uendeshaji, katika mazingira hayo haitawezekana kuwepo huduma zenye ufanisi,” anasema.

“Wanagoma kuongeza nauli, wanataka huduma bora, hawatoi ruzuku kwa wakala, unadhani ufanisi utatoka wapi?” kimehoji chanzo hicho ndani ya Temesa.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kinachokwamisha baadhi ya mambo, ikiwemo kuongezwa nauli ni sababu za kisheria.

Kifungu cha 5 cha Sheria ya kuanzishwa kwa Temesa ya mwaka 2005, inamtaja Waziri wa Ujenzi kuwa ndiye mwenye mamlaka ya juu kwa Temesa.

Kwa tafsiri ya sheria hiyo, Waziri wa Ujenzi (Innocent Bashungwa kwa sasa), ndiye mwenye mamlaka ya kupanga nauli za vivuko.

Nyaraka ziliyopatikana katika uchunguzi wa Mwananchi, zinaonyesha kuwapo pendekezo la ongezeko la nauli ya vivuko iliyowasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wakati huo, (Profesa Makame Mbarawa) ambaye alikataa kulibariki.

Sababu nyingine ya mkwamo wa kuongeza nauli imebainika ni masilahi ya kisiasa ya viongozi serikalini.

Chanzo kingine ndani ya wakala huo kinasema, “wanakwambia kule Kigamboni kuna wapigakura wengi, ukipandisha nauli utawagombanisha viongozi na wananchi wao, kwa hiyo ibaki hivi hivi kwanza.”

“Kwa sababu mwenye mamlaka ya kuamua ongezeko la nauli ni waziri ambaye kimsingi ni mwanasiasa, anafanya maamuzi kwa kuangalia masilahi ya kisiasa, si uhai wa wakala,” anasema.

Akizungumzia nauli, Kilahala alikiri kutoongezeka nauli kwa takribani miaka 12 na kwamba Temesa ilishawahi kuomba ongezeko hilo.

Hata hivyo, anasema mabadiliko ya nauli yatatokana na tathmini ya kitaalamu ambayo hivi karibuni timu itaundwa kuifanya.

“Katika nyakati hizo ni muhimu wananchi waendelee kupata huduma, huku tathmini ikifanyika, hii timu ndiyo itatupa jawabu la kiwango gani kinapaswa kiongezeke,” anasema.

Vivuko vya Azam mzigo mwingine

Mbali na ufinyu wa mapato, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023, anabainisha mengine yaliyojificha kuhusu malipo ya kukodi vivuko.

Ripoti ya CAG inabainisha Temesa inalipa Sh5 milioni kila siku kwa Azam Marine Ltd kama gharama ya ukodishaji wa vivuko vya Sea Tax 1 na Sea Tax 2.

Kutokana na gharama hizo, CAG Charles Kichere kupitia ripoti hiyo, anasema wakala ulilipa Sh1.8 bilioni kwa mwaka kwa Azam Marine Ltd kwa ajili ya ukodishaji huo kuanzia Julai mosi, 2022 hadi Juni 30, 2023.

Kiasi ambacho Temesa imeilipa Azam Marine Ltd ni theluthi moja ya jumla ya mapato ya mwaka yaliyotokana na vivuko vyote vya Kigamboni-Magogoni ambayo ni Sh5.76 bilioni.

Temesa ilibakiwa na Sh3.93 bilioni kwa ajili ya kugharimia uendeshaji, yakiwamo mafuta ya vivuko, gharama za kazi, ukarabati na matengenezo. Hata hivyo, fedha hizo hazikutosheleza mahitaji kwa mujibu wa ripoti ya CAG.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini katika kila abiria anayepanda Sea Tax 1 (inayobeba abiria 250), Temesa inailipa Azam Marine Ltd Sh300.

Temesa inalipa fedha hizo ilhali kiasi inachokusanya kwa abiria hao magetini ni Sh200. Hivyo inatumia Sh100 kutoka vyanzo vingine kuongezea nauli ya kila abiria anayepanda Sea Tax.

Si hivyo tu, bado Temesa inawajibika kulipa Sh300 kwa kila abiria, wakiwemo wanafunzi na maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, ambao katika mageti hawatozwi nauli yoyote.

Mkurugenzi wa Temesa, Kilahala ameieleza Mwananchi kuwa kukodishwa kwa vivuko hivyo kulilenga kuongeza huduma, baada ya Mv Magogoni kwenda kwenye matengenezo.

“Kwa sababu mahitaji ni makubwa ndiyo maana tumekodi vivuko hivyo, lakini kinachoagaliwa zaidi ni huduma kwa wananchi,” anasisitiza.

Alipotafutwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuzungumzia hayo, alijibu atafutwe Mtendaji Mkuu wa Temesa.

“Mwandishi naomba uwasiliane na Mtendaji Mkuu wa Temesa kwa ufafanuzi zaidi wa maswali yako,” amejibu Bashungwa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (sms).

Related Posts