Wabunge walia na malimbikizo madeni ya watumishi wa umma

Dodoma. Wakati wabunge wakihoji malimbikizo ya madeni ya mishahara na stahiki nyingine za watumishi wa umma, Serikali imesema imetumia Sh219 bilioni kulipa madeni ya mishahara yaliyoanza Mei 2021.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Neema Mgaya leo Mei 27, 2024, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti uzalishaji wa madeni ya watumishi, yakiwemo malimbikizo ya mishahara.   

Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kujenga Mfumo Mpya wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ulioanza kutumika Mei 2021, ambao umedhibiti uzalishaji wa malimbikizo mapya ya mishahara.

 “Pamoja na hatua hiyo, kuanzia Mei, 2021 hadi sasa Serikali imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 132,611 yenye thamani ya Sh219.73 bilioni,”amesema.

Aidha, ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuhakiki na kuwasilisha madeni ya watumishi kwa ajili ya taratibu za uhakiki na malipo.

Katika swali la nyongeza Neema amehoji Serikali imejipanga vipi na lini itakamilisha ulipaji wa madeni.

Pia amesema walimu wamekuwa wakilipwa madeni yao kupitia halmashauri, hivyo akahoji Serikali imejipanga vipi kuhakikisha inapeleka fedha hizo kwenye halmashauri ili walimu walipwe madeni yao.

Akijibu maswali hayo, Ridhiwan amesema kwa mujibu wa taratibu walizojipangia wanataka kuhakikisha madeni hayo ikiwezekana yanakamilika hata leo.

“Sisi kwetu kinachotukwamisha, wale waajiri ambao hawaleti taarifa kwa wakati. Nawasihi wabunge wenzangu tuendelee kuwasisitiza waajiri hasa wakurugenzi walete taarifa za madai ya watumishi ili tuweze kukamilisha kilio hiki,” amesema.

Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Oscar Kikoyo amezungumzia askari waliopigana vita vya Uganda mwaka 1978 hadi 1979,  akihoji ni lini Serikali itawalipa stahiki zao.

Hata hivyo, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson aliingilia kati na kusema tayari ameshaiagiza Serikali kulifanyia utafiti jambo hilo kwa ujumla na wanaendelea nalo.

“Nadhani wakishalihitimisha watalileta ili tujue kama kipo wanachokidai au walishalipwa, lakini kama unataka kuuliza kama swali la msingi unaruhusiwa, kwa maana ya Serikali, Bunge lilishatoa agizo kwa Serikali lilifanyie utafiti jambo hili,” amesema Spika.

Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amesema kada ya wauguzi wanadai fedha nyingi na kuhoji ni lini Serikali itawapatia fedha zao.

Akijibu swali hilo, Ridhiwani amesema wao wanafanya kazi kwa taarifa na kuwataka waajiri wote nchini kuwasilisha madeni ya watumishi kwa wakati ili waweze kulipwa.

Suala hilo pia limemwibua Tunza Malapo, mbunge wa Viti Maalumu akihoji ni lini Serikali itawalipa walimu ambao madeni yao yamehakikiwa lakini hawajalipwa.

Akijibu swali hilo, Ridhiwani amewataka wabunge kuwasisitiza waajiri wapeleke taarifa za madeni ya watumishi kwenye ofisi yake na kuwa watazifanyia kazi.

Baada ya majibu hayo, Spika Tulia amembana na Ridhiwani akimtaka aeleze iwapo kuna fedha za kuwalipa watumishi wanaoidai Serikali, pindi wabunge watakapoleta taarifa zao.

Akijibu swali hilo, Ridhiwani amesema fedha zipo za kuwalipa watumishi wa Serikali, wanaodai madeni.

Baada ya mjadala huo, Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema Serikali itakachokifanya baada ya kupokea taarifa za watumishi wanaoidai Serikali ni kufuatilia kuona ni makundi gani ambayo yamekuwa na changamoto za muda mrefu.

 “Kwa sababu tunachojua fedha zinaweza kuwepo, lakini waajiri na wasimamizi wa watumishi wamekuwa wakifanya ndivyo sivyo katika kuhakikisha madai ya watumishi yanalipwa kwa kuzingatia mifumo na taratibu tulizoziweka,” amesema.

Related Posts