MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba na Singida Fountain Gate, Meddie Kagere ni miongoni mwa wachezaji watatu wanaotajwa kwamba huenda wakakatwa wakati wa dirisha lijalo.
Inaelezwa kwamba tayari uongozi wa timu hiyo umeanza kusaka mbadala wa wachezaji hao ambapo mbali na Kagere aliyekuwa anaichezea kwa mkopo wa miezi sita, pia kuna Pius Buswita na Derick Mukombozi ambao mikataba yao imeisha.
Ishu ya Kagere wapo viongozi wanaotamani aendelee kuwapo kikosini, lakini rekodi ya mabao akiwa amefunga moja ndani ya timu hiyo inawatatiza.
Nje na viongozi hao, hivi karibuni Mwanaspoti lilifanya mazungumzo na kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera aliyesema anataka kuboresha safu ya ushambuliaji kwani ina ubutu wa kufunga mabao.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya timu kinasema: “Baada ya kumaliza mechi yetu dhidi ya Tabora United, tutajua tunawaacha wachezaji wangapi na wangapi watasajiliwa.”
Buswita anayeongoza kwa mabao matano ndani ya kikosi hicho anahusishwa kutakiwa na KMC na Coastal Union ya Tanga, lakini mchezaji huyo amefafanua hilo akisema: “Kuna timu nyingi zinahitaji huduma yangu, ila kwa sasa acha kwanza nimalize mechi ya mwisho, ili nipate muda wa kutafakari msimu ujao nitakuwa wapi.”
Kwa upande wa Kagere hakuwa tayari kuzungumzia hatima yake Namungo na huenda baada ya kumalizana na Tabora United atakuwa tayari kuweka wazi.