Katavi. Watu saba wamefariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupasuka kisha kupinduka Halmashauri ya Mlele, Kitongoji cha Lungunya mkoani Katavi.
Vifo hivyo vimetokea hii jana Jumapili, Mei 26, 2024 ambapo inaelezwa mtumbwi ulikuwa umebeba watu 14 na magunia 10 ya mpunga hivyo ukashindwa kuhimili uzito huo.
Hadi usiku wa jana ni mwili mmoja umepatikana huku juhudi zaidi zikiendelea kuipata mingine sita.
Kitongoji cha Lungunya wanatumia mitumbwi kusafiri kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kuharibu miundombinu ya barabara.
Mkazi wa eneo hilo, Shija Mwakahema ameiomba Serikali kukaa chini na kuangalia suala hilo kwani mafuriko yanaendelea na yataendelea na kuiomba Serikakali kukaa chini na kuliangalia suala hilo.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Katavi, Lilian Wanna alisema katika tukio hilo wamefanikiwa kutoka watu saba kati ya 14 waliokuwa wakisafiri.
“Asubuhi tumefanikiwa kupata mwili mmoja huku miili mingine sita bado haijapatikana,” alisema Kamanda Lilian.
Alisema wanaendelea kuwatafuta huku changamoto ikiwa eneo hilo la bonde kuwa na mamba pamoja na viboko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele kufanywa tathmini ya eneo hilo kama bado ni salama kuishi ili kufahamu maji yaliyopo hapo yanatoka wapi.
“Tukisema hapa hapafai kwa maisha ya mwanadamu basi mtuelewe, pia mchukue tahadhari kwa ajili ya kuepukana na vifo,” alisema.