Waziri wa Kazi atembelea Mtibwa Sugar, aitaka OSHA kukamilisha uchunguzi wa ajali

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi, ametembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mtibwa kufuatia ajali iliyotokea Mei 22, 2024 ambapo ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kukamilisha uchunguzi wa ajali hiyo ili kuruhusu kiwanda hicho kurejea katika uzalishaji kwa haraka.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi pamoja na Wakuu wa Taasisi za OSHA na WCF pamoja na Wakaguzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi wa OSHA wakipokea maelezo kutoka kwa Meneja Msaidizi wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, Juma Saidy (mwenye shati yenye mistari myekundu) juu ya nama ajali ilivyotokea na kusababisha vifo vya watu 13 Kiwandani hapo.

Waziri Ndejembi ametoa agizo hilo Mei 26,2024 mara baada ya kutembelea eneo la ajali na kupatiwa maelezo kuhusu ajali hiyo na uongozi wa kiwanda pamoja na taarifa ya awali ya uchunguzi kutoka OSHA.

“Nitumie nafasi hii kutoa pole kwa uongozi wa kiwanda kutokana na athari kubwa za ajali hii iliyogharimu maisha ya wataalam 13 pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiwanda. Aidha, niseme tu kwamba huu sio wakati wa kumtafuta mchawi bali ni wakati wa kufanya uchunguzi na tafakari ya kina ili kung’amua chanzo cha tatizo lililojitokeza kwa minajili ya kufanya maboresho yatakayozuia janga kama hilo au mengine kujitokeza tena. 

“Aidha, nizipongeze Taasisi chini ya Ofisi yangu zinazohusika katika suala hili hususan OSHA kwa kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia jambo hili na niwatake kukamilisha taarifa ya uchunguzi wa ajali hii haraka sana ili kuruhusu maboresho ya miundombinu ya kiwanda kufanyika na uzalishaji kuendelea kuepuka athari zaidi kiuchumi kutokana na uzalishaji wa sukari kutofanyika hasa tukizingatia kwamba kiwanda hiki kinategemewa na wakulima wengi ambao huuza miwa yao hapa,” amesema Ndejembi.

Akimwelezea Waziri jinsi ajali ilivyotokea, Meneja Msaidizi wa Kiwanda, Juma Saidy, amesema ajali hiyo ilitokea wakiwa wanafanya makabidhiano ya mtambo wa kufua umeme kwa njia ya mvuke (steam turbine) wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 15 za umeme kutoka kilowati 6 za awali lengo likiwa kuongeza uzalishaji wa sukari.

Kwa mujibu wa Saidy mtambo huo ulikuwa unalishwa na mtambo mpya wa kufua mvuke Na. 4 (Steam Boiler No.4), wenye uwezo wa kuzalisha mvuke wa tani 125 kwa saa na kiwango cha mkandamizo (pressure) wa bar 45 ambapo joto linaloweza kuzalishwa linafikia nyuzi joto 450 0C. 

“Majira ya saa saba usiku wa kuamkia tarehe 23.05.2024 wakati zoezi la makabidhiano yanayotokana na kubadilisha mfumo wa awali wa kufua umeme yakiendelea, ndipo ajali ilipotokea katika eneo la mtambo wa kuzalisha umeme (power house),” ameeleza Saidy. 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema tathmini ya awali iliyofanywa na wataalam wake ambao walifika katika eneo la tukio tangu Mei 23 inaonyesha chanzo cha ajali ni kupasuka kwa kiungio (bellow) ambacho ni sehemu ya mfumo wa uhimilivu wa mitetemo (Gimbal Expansion Joint). 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akieleza hatua zilizochukuliwa na taasisi ya OSHA baada ya ajali kutokea katika Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa Mei 22, 2024 ambapo amebainisha kuwa tayari Wataalamu wa OSHA watakabidhi ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo kwa Waziri mapema wiki hii.

Ameongeza kuwa mpasuko huo ulipelekea kufumuka kwa kiungio hicho kutokana na msukumo mkubwa wa mgandamizo wa mvuke ambao ulipelekea vifo vya papo hapo kwa wafanyakazi 11 na majeruhi wawili ambao walifariki dunia Mei 24,2024 wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma. 

Aidha, ameahidi kuwa wataalam wake watakamilisha uchunguzi huo haraka iwezekanavyo na kutoa ushauri wa kina juu ya maboresha yanayohitajika katika kuzuia changamoto iliyotokea kujirudia au changamoto nyingine kutokea.

Pamoja na taarifa hiyo ya awali kuhusiana na ajali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, amewataka wamiliki wa sehemu za kazi kufuata taratibu na miongozo ya usalama na afya kazini ikiwemo kutoa taarifa OSHA kuhusu maboresho wanayofanya au miradi mipya katika maeneo yao ili waweze kushauriwa ipasavyo juu ya kanuni bora za kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vitokanavyo na miradi au maboresho husika.

Related Posts