Zanzibar yasajili laini za simu 849,000

Unguja. Zanzibar imesajili laini za simu za mezani na mkononi 849,082 sawa na kadirio la watumiaji 446,885. 

Kati ya laini hizo, idadi ya watumiaji wa simu za mkononi ni 439,470 na simu za mezani ni 7,415 ambao ni sawa na asilimia 23.6 na asilimia 0.4 ya wakazi wa Zanzibar. 

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina jumla ya watu milioni 1.8.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Yussuf ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Mei 27, 2024 wakati akijibu swali la mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kujua idadi ya wananchi wanaotumia simu na huduma za intaneti. 

Katika majibu yake, Nadir amesema taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya robo mwaka inayoishia Machi, 2024 kuhusu takwimu za mawasiliano, idadi ya watumiaji waliosajili kwa ajili ya huduma za intaneti ni 463,322 sawa na kadirio la watumiaji 330,946 ambao ni sawa na asilimia 17.5 ya wakazi wa Zanzibar. 

“Hali hii ya kukua kwa uchumi wa kidijitali inaonekana kwa mafanikio ya sekta zote zimehamia kwenye kujiendesha na kutoa huduma kupitia mitandao ya simu na intaneti,” amesema.

Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na Serikali mtandao (e- office), huduma za kuunganisha mikonga ya Taifa (wifi cables), kufungua barua pepe za Serikali (e-government), huduma za malipo kwa kutumia mitandao ya laini  za simu za mkononi na intaneti (E-Banking, E-insurances), lipa kwa simu, huduma za maji, umeme na ving’amuzi.

Hata hivyo, alikiri kutokana na kuimarika kwa huduma za mitandao ya simu na intaneti kumejitokeza baadhi ya changamoto katika zikiwamo kuripotiwa kwa matukio ya ulaghai, uhalifu mtandaoni. 

Hata hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vinaitambua changamoto hiyo na kuchukua hatua pindi uhalifu unapotokea pia wataendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujiepusha na uhalifu huo wa mitandaoni.

Related Posts