Allaince One yatokomeza uhaba wa maji Urambo

 

Na Mwandishi Wetu,Urambo

Wakazi zaidi ya 6000 wa Kitongoji cha Kitega Uchumi wilaya ya Urambo mkoani Tabora wameondokana na changamoto ya maji baada ya Kampuni ya Tumbaku ya Alliance one kuwajengea kisima cha maji safi na salama katika kitongoji chao.
Kisima hicho kilichogharimu zaidi ya shilingi milioni 34 kitahudumia Kaya 671 za eneo la Kitega uchumi ambazo awali zililazimika kufuata huduma ya maji umbali mrefu na gharama kubwa kutokana na uhaba mkubwa wa maji katika eneo hilo.
Akizindua kisima hicho, Mkuu wa wilaya ya Urambo kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi Elibariki Bajuta pamoja na kuipongeza Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One kwa kukisaidia kitongoji hicho kupata huduma ya maji ameiomba pia kusaidia zaidi katika sekta ya uchumi.

Bajuta amewaonya viongozi wa Kitongoji hicho kutowatoza fedha Akina mama wanaochota maji, na kwamba Kampuni iliyochimba kisima imetoa huduma hiyo bure kwa Wakazi wa eneo hilo na amewataka kukitunza kisima hicho ili kiendelee kudumu kwa muda mrefu.

“Nikipata taarifa zozote za malalamiko kutoka akima mama hawa kuwa wamelipishwa hela za maji..nitaanza na Mwenyekiti wa Kitongoji, nitakupumzisha sehemu salama wakati nashughulikia tatizo lako, nafikiri mnanifahamu huwa siongea jambo mara mbili´alionya Mkuu huyo wa wilaya.

Mkurugenzi wa uzalishaji wa Kampuni ya Alliance one David Mayunga amesema kampuni hiyo ina utaratibu wa kuchangia huduma za jamii katika maeneo inayonunua tumbaku hasa katika sekta za Afya, Mazingira na Elimu, na kwamba Kisima hicho ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wao.

“Kabla ya kuchimba kisima hiki tulifanya utafiti na kubaini tatizo la maji katika kitongoji cha Kitega uchumi ndipo tukaamua kuchimba kisima chenye urefi wa mita 150 kwenda chini, kujenga mnara wa Tenki la maji pamoja na usambazaji, kazi zilizogharimu kiasi hicho” alisema Mayunga.

Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira wilaya ya Urambo Petro Kisasi amesema upatikanaji wa maji katika mji wa Urambo ni asilimia 24.5 na uzalishaji unategemea visima virefu saba ambavyo uwezo wake ni kuzalisha maji mita za ujazo 388 kwa siku, wakati mahitaji ni lita milioni 3.6 kwa siku.

Baadhi ya Wananchi wa Kitongoji Kitega uchumi, Rosemarry Yusuph ameishukuru Kampuni hiyo kwa kuwaondolea kero kubwa ya maji Katika eneo hilo na kwamba hivi sasa wana uhakika wa kutumia maji salama na bila gharama yoyote.
Asia Athumani akielezea adha waliyokuwa nayo ya kwenda kuteka maji ya kunywa katika kijiji cha jirani cha Kilimahewa ambako walikuwa wananunua ndoo moja kwa shilingi 50.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kitega uchumi Fredrick Alloyce amesema awali Wananchi wake walikuwa watumia maji ya visima vifupi ambavyo sio salama kwa matumizi ya kunywa, hivyo walikuwa wanayatumia kufulia na kuoshea vyombo.
“Kwa kweli Kampuni hii imewakomboa akina mama, hata sisi akina baba maana muda mwingi tuliutumia kutafuta maji tena kwa kuyalipia, lakini hivi sasa tumepata maji salama na bure..naomba makapuni mengine yafanye kama Alliance One” alisema Mwenyekiti huyo wa kitongoji.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ya Urambo amezitaka Kampuni za ununuzi wa Tumbaku kuhakikisha zinawalipa Wakulima ndani ya wiki mbili baada ya kuchukua Tumbaku zao, na kwamba hatasita kukamata magari na kufunga milango yote ya ofisi ya Kampuni itakayoshindwa kufanya hivyo katika wilaya yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uzalishaji wa Kampuni ya Alliance One(AOTL) David Mayunga ametoa rai kwa Wakulima wote wa Tumbaku, kuboresha kilimo na kutunza Tumbaku ili kupata madaraja mazuri na kupata mapato mazuri na kufunga tumbaku vizuri bila kuchanganya madaraja maarufu kama Ngulai.

Pia amewaasa Wakulima wa Tumbaku kuepuka kuwatumikisha watoto katika mashamba ya tumbaku, kuacha tabia ya kuchanganya tumbaku na vitu visivyo Tumbaku, kupanda na tunza miti inayoendana na kilimo cha tumbaku na kulinda mazingira kwa ujumla.

“Tunasisitiza Wakulima kuzingatia taratibu hizo kwa manufaa yenu wenyewe, maana tukigundua tatizo kwenye mabelo ya Tumbaku tunareject yote, hiyo inakuwa ni hasara kubwa kwa Wakulima” alisisitiza Mkurugenzi huyo na kuwataka Wakulima kutojaribu kufanya hivyo.

Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Allaince One, David Mayunga(Kulia) akisaidiana Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti(Kushoto)  kumtwisha ndoo ya maji Bi.Tausi Juma, mkazi wa Urambo mara baada ya kampuni hiyo kukabidhi kisima cha maji kwenye kitongoji cha  Kitega Uchumi wilayani humo.


Mkuu wa Wilaya ya Urambo Bw Elibariki Bajuta (Wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Allaince One, David Mayunga(Wa tatu Kulia) akimtwisha ndoo ya maji Amina Saidi mkazi wa Urambo mara baada ya kampuni hiyo kukabidhi kisima cha maji kwenye kitongoji cha Kitega Uchumi wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Urambo,Elibariki Bajuta (Kulia) akitata utepe ili kuzindua kisima cha maji kilichotolewa na Kampuni ya Alliance One kwa wakazi wa kitongoji cha Kitega Uchumi wilayani humo,huku Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti (Kushoto) akishuhudia.


Mkuu wa Wilaya ya Urambo Bw.Elibariki Bajuta(Wa Katikati walioketi), Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Allaince One, David Mayunga(Wa kwanza kushoto walioketi) na Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti(Wa kulia walioketi) wakiwa katika picha ya pamoja na wanufaika kisima cha maji ambacho kimetolewa msaada na kampuni hiyo mara baada makabidhiano yaliyofanyika kwenye kitongoji cha Kitega Uchumi wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Urambo Bw Elibariki Bajuta(Wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Allaince One, David Mayunga(Wa tatu Kulia) akimtwisha ndoo ya maji Amina Saidi mkazi wa Urambo mara baada ya kampuni hiyo kukabidhi kisima cha maji kwenye kitongoji cha Kitega Uchumi wilayani humo.

Related Posts