Atupwa jela miaka 30 kwa kuwabaka watoto watatu

Morogoro. Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro imemhukumu kifungo cha miaka 90 ,  mkulima Leonce Athanas Matea maarufu kwa jina la Alaji (55), mkazi wa Chicago A’ Kata ya Kidatu wilayani humo,  baada ya kumtia hatiani kwa makosa matatu ya ubakaji wa watoto watatu.

Hata hivyo, mkulima huyo atatumikia kifungo hicho  kwa miaka 30, kwa kuwa adhabu hiyo itaenda pamoja.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Mei 27, 2024 na Hakimu  Bestina Saning’o  baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka,  uliothibitisha mashtaka yote matatu dhidi ya mshtakiwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria yaani bila kuacha shaka yoyote

Awali, baada ya mahakama kumtia hatiani mshtakiwa huyo, mwendesha mashtaka, Mkaguzi wa Polisi,  Thomas Kamsini aliiomba mahakama  itoe adhabu kali kwa mshtakiwa hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo za kubaka watoto wadogo.

Alaji aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu akidai umri wake umeenda.

Hata hivyo, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, Hakimu Saning’o alimtia hatiani mshitakiwa huyo kwa kumfunga kifungo cha miaka 30 kwa kila kosa alilokuwa anashitakiwa nalo.

“Baada ya kumtia hatiani kwa makosa matatu ya ubakaji wa watoto kama alivyoshtakiwa,mahakama hii inamhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kila kosa kwa mujibu wa sheria,” amesema Hakimu Saning’o.

Hakimu Saning’o amesema adhabu zote katika mashtaka yote matatu zitakwenda kwa pamoja,  hivyo mshtakiwa atatumikia adhabu ya kifungo hicho kwa kuishi gerezani kwa miaka 30.

Baada ya Hakimu Saning’o kusoma hukumu hiyo mhalifu huyo alichukuliwa na kupelekwa katika gereza la Kiiberege kuanzia kutumikia adhabu yake hiyo.

Saning’o alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 24, 2023 na kusomewa mashitaka hayo matatu ya ubakaji wa watoto watatu tofauti ambao wote majina yao yanahifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Katika shitaka la kwanza, mshtakiwa alidaiwa  kati ya Juni Mosi, 2023 na Novemba 16, 2023 katika Kijiji cha Chicago, Kata ya Kidatu Wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro, alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka tisa.

Katika shitaka la pili tarehe hiyo hiyo na sehemu hiyo hiyo, alimbaka mtoto mwingine wa miaka 10 na katika shitaka la tatu alidaiwa kati ya  Novemba Mosi, 2023 hadi Novemba 16, 2023  alimbaka mtoto mwenye miaka mitano.

Mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo na upande wa mashtaka katika kuthibitisha mashtaka hayo,  uliwaita mashahidi 12 wakiwemo  waathirika.

Kwa mujibu wa ushahidi wao mshitakiwa huyo alikuwa akiwarubuni watoto hao kwa kuwaita ndani ya nyumba yake na kuwafanyia kitendo hicho kwa zamu kisha kuwapa Sh200 kila mmoja.

Related Posts