Aziz Ki abeba tuzo ufungaji bora Bara 2023/24

DAKIKA za jioni kabisa. Vita imeisha. Stephane Aziz Ki wa Yanga ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara katika mechi ya mwisho wa msimu akimzidi kete Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam.

Ni vita kali ambayo ilichagiza ushabiki kwenye mechi za jana jioni hususani kwenye vibandaumiza.

Aziz Ki ndiye ameibuka mbabe wa vita hiyo iliyoteka hisia za wengi baada ya kumaliza ligi akiwa kinara wa mabao akifunga 21, huku Fei Toto akifunga 19.

Michezo ya mwisho ndiyo imetoa mshindi wa vita hiyo ambapo Aziz Ki na Fei Toto ambao ni maswahiba wakubwa nje ya uwanja, waliingia katika mzunguko wa 30 kila mmoja akiwa na mabao 18 mkononi.

Wakati wawili hao wakiwa sawa kwa mabao, wengi walikuwa wakijiuliza itakuwaje kama wakimaliza hivyohivyo, lakini kanuni ilikuwa inaondoa utata juu ya mjadala huo.

Kanuni ya (13:1) kuhusu mshindi wa Tuzo ya Mfungaji Bora inaeleza, ikiwa wachezaji zaidi ya mmoja wamefungana idadi ya mabao njia ya kwanza itakayotumika wataangalia mabao yaliyofungwa kwa njia ya kawaida yatapewa alama mbili (2).

Mabao yatakayofungwa kwa njia ya penalti yatapewa alama moja (1) na ikiwa watalingana pia itatumika kanuni ya (13:2) inayoelezea mchezaji aliyecheza dakika chache atakuwa mshindi na ikitokea wakalingana pia itaangaliwa kanuni ya (13:3). Kanuni hiyo ya (13:3) inaeleza, kama vigezo vyote vilivyowekwa vinafanana pia basi, nyota aliyefunga mabao mengi ugenini atakuwa mshindi. Kutokana na hilo, wakati nyota hao walipokuwa na idadi sawa ya mabao Aziz Ki alikuwa amefunga penalti tatu huku Fei Toto akiwa amefunga moja.

Aziz Ki amefanikiwa kuishinda vita kwa kumpiku Fei Toto mabao mawili baada ya kuongoza maangamizi mbele ya Tanzania Prisons kwa ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Aziz Ki alifunga dakika ya 11 kwa mkwaju wa faulo moja kwa moja iliyotokakana na yeye mwenyewe kuchezewa vibaya nje kidogo ya eneo la hatari la Tanzania Prisons. Bao la pili alifunga dakika ya 12 akimalizia pasi ya Kennedy Musonda.

Mabao hayo mawili ya harakaharaka yaliyofungwa na Aziz Ki, yalikuja baada ya Tanzania Prisons kuwa mbele mapema tu dakika ya tano mfungaji akiwa Beo Ngassa. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Yanga kuongoza 2-1. Kipindi cha pili, Kennedy Musonda aliongeza bao la pili kwa kichwa dakika ya 52. Aziz Ki alihitimisha ushindi kwa kufunga dakika ya 80 akimalizia pasi ya Clement Mzize.

Kwa kitendo cha Aziz Ki kuwa kinara wa mabao akifunga 21, anaingia kwenye listi ya wafungaji bora wa ligi hiyo waliofunga mabao 20 na kuendelea kama ilivyokuwa kwa Emmanuel Okwi (Simba – 20), Meddie Kagere (Simba – 23 na 22), Abdallah Juma (Mtibwa SUgar – 25), huku mbabe wao ni Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu Tanzania akifunga mabao 26, rekodi hiyo aliiweka mwaka 1997 akiwa anaitumikia Yanga.

Aziz Ki ameifikia rekodi ya Amissi Tambwe aliyefunga mabao mengi (21) katika ligi ndani ya Yanga akifanya hivyo msimu wa 2015-2016.

Timu alizozifunga na aina ya mabao:
Agosti 23, 2023 -KMC dakika 59 (mguu wa kushoto).
Agosti 29, 2023- JKT TZ dakika 50, friikiki (mguu wa kulia)
Oktoba 7, 2023-Geita Gold dakika 48 (mguu wa kulia).
Oktoba 23, 2023 hat-trick -Azam FC dakika 9 (friikiki mguu wa kulia), dakika 69 na 72 (mguu wa kushoto)
Novemba 5, 2023-Simba dakika 73 (mguu wa kushoto)
Desemba 16, 2023- Mtibwa Sugar P-dakika 45, 64 (mguu wa kushoto)
Desemba 23, 2023- Tabora United dakika 21 (frikikii mguu wa kushoto)
Machi 8, 2024- Namungo FC dakika 63 (mguu wa kushoto)
Machi 11, 2024- Ihefu dakika 68 (mguu wa kushoto)
Machi 14, 2024- Geita Gold dakika 54 (mguu wa kulia)
Aprili 14, 2024- Singida FG dakika 66 nje ya 18 (mguu wa kushoto)
Aprili 20, 2024- Simba penalti dakika 20 (mguu wa kushoto)
Mei 22, 2024) -Dodoma penalti dakika 45, dk 51 (mguu wa kushoto).
Mei 25, 2024) – Tabora United dakika ya 90+1 (kichwa)
Mei 28, 2024) – Tanzania Prisons dakika ya 11 (friikiki mguu wa kushoto), dakika ya 12 na 80 (mguu wa kushoto).
 

Related Posts