Bei vocha za simu zapanda kinyemela, TCRA CCC waonya

IMEBAINIKA kuwa bei za vocha za kampuni mbalimbali za mitandao ya simu zimepandishwa bei kinyemela katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Mbeya, Songwe na Rukwa. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe … (endelea).

Katika ufuatiliaji uliofanywa na Mtandao wa MwanaHALISI Online katika maduka mbalimbali kwenye mikoa hiyo, umebaini kuwa bei za vocha za Sh 500 kwa sasa zimepanda na kuuzwa kwa Sh 600,  vocha za Sh 1,000 zinauzwa Sh 1,200, wakati vocha za Sh 2,000 zinauzwa Sh 2,400.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti wamesema kuwa kitendo cha wauzaji wa vocha za kukwangua kupandisha bei kimechangia kwa kiasi kikubwa wananchi kushindwa kuwasiliana na ndugu zao hasa wanaoishi vijijini ambako hakuna maduka ya kutoa pesa.

Mmoja wa wananchi hao, ni Michael Mbugh ambaye ni Mkazi wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe amesema kuwa maeneo mengi mkoani humo hakuna sehemu za kukufanya miamala ya pesa hivyo wananchi wanategemea zaidi vocha za kukwangua na sio za kurushiana miamala kwa njia ya simu.

”Wapo wengine ambao wanadai kuwa ni bora waweke kwenye simu zao ili wajiunge wenyewe lakini ukweli ni kwamba vijijini wengi hawana elimu hiyo hivyo wanachokijua ni vocha za kukwangua,” amesema Mbugh.

Ameongeza kuwa wanachokifanya wauza vocha ni kuwachonganisha wananchi na Serikali ambapo hivi sasa wanadai kuwa Serikali imeongeza bei bidhaa mbalimbali hadi kwenye vocha.

Naye Steven Jonas ambaye ni Mkazi wa Mbalizi mkoani Mbeya amesema kitendo cha kuongeza bei kwenye vocha kinyemela kimewachanganya wananchi ambao wanakipato kidogo.

Steven amesema wapo wananchi ambao vocha ya Sh 500 kuipata ni shida kwao hivyo anashindwa hata kuwasiliana na ndugu aliyeko mjini.

“Wananchi wenye kipato kidogo wanapata shida sana na hili ongezeko la bei za vocha, ni dhahiri inawaumiza sana wananchi,” amesema Steven.

Akizungumzia kuhusu ongezeko la bei, Msemaji wa Kampuni Airtel Tanzania Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Johnson Mbwambo amesema kuwa walioongeza bei ni wahujumu uchumi na wezi hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mbwambo amesema kampuni hiyo itafanya msako wa kuwakamata watu wote na kwamba iwapo ni mawakala ambao ndio wamepandisha bei za vocha kampuni hiyo itawachukulia hatua za kisheria mawakala wao.

“Sisi Airtel hatujaongeza bei za vocha kiasi cha wauzaji wa bei za rejareja kupandisha hadi kiasi cha Sh 100, 200 hadi 400 huo ni wizi mkubwa na ni hujuma wanaifanya ili watu waichukie serikali” amesema Mbwambo.

MwanaHALISI Online imemtafuta msemaji wa kampuni ya Vodacom Tanzania Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Baraka Musabula ambaye amesema kuwa kampuni hiyo itawasiliana na vyombo vinavyohusika na masuala ya mitandao ili kuona namna ya kuwachukulia hatua.

Musabula amesema vocha za aina yeyote haijawahi kuwa na faida ya Sh 100 na iwapo wauzaji wanaona kuwa hawapati faida bora waachane na kuuza vocha kuliko kufanya hujuma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa kwa sasa watatumia radio kutangaza ili wanaofanya hujuma ya bei hizo ujumbe uwafikie na iwapo wataendelea kufanya hujuma hiyo wakamatwe.

Aidha, amesema ni jambo baya kufanya hujuma ya aina hiyo na kwamba wananchi lazima wataichukia serikali kutokana na ongezeko la bei ambayo haistahili.

“Sisi hatuwezi kupandisha bei za vocha hivyo tunaomba wananchi watoe taarifa kwa mtu yeyote ambaye atapandisha vocha, pia watoe ushirikiano kuwavumbua wote ambao wanawapandisha bei za vocha.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC), Mary Shao Msuya

“Wanaopandisha bei ni sawa na wezi wengine hivyo hawapaswi kuwafumbia macho lazima wachukuliwe hatua” ameongeza Baraka.

Baraka amesema bei kwa sasa ziliongezeka kidogo kwani vocha ya Sh 1,000 imeongezwa Sh 15 tuu na kuongeza kuwa hakuna vocha ambayo inazidi kiasi cha Sh 100.

Kwa upande wake msemaji wa Kampuni za Tigo Zantel Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Woinde Swai alipozungumza na MwanaHALISI Online alisema kuwa taarifa za kupanda au kushuka kwa bei atatoa taarifa kupitia barua pepe.

MwanaHALISI ilifika katika ofisi za Tigo Kanda ya juu kusini ambapo ilikutana na mmoja wa maofisa waandamizi wa kampuni hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kile alichokisema kuwa sio msemaji wa kampuni. Hata hivyo, alikiri kuwa kweli vocha zote zimepanda bei.

Afisa huyo amesema muda si mrefu vocha zote zinapanda bei na sasa zimepanda bei kwa kuwa hata TTCL nao wamepandisha bei.

Aidha, mmoja wa mawakala wanaouza vocha mkoani Songwe, Julius Mtafya amesema sababu kubwa ya kupandisha bei za vocha hizo ni faida kiduchu wanazozipata kwenye mauzo ya vocha hizo.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC), Mary Shao Msuya amesema vocha ya kampuni yoyote ya mawasiliano ina bei elekezi hivyo inatakiwa inunuliwe kwa bei hiyo.

Amesema kama vocha ya ni ya 1,000 inatakiwa kuuzwa kwa bei hiyohiyo hivyo kinachofanyika sasa ni wizi.

“Hata mikoa ya Lindi na Mtwara baadhi ya maeneo tumepata malalamiko kwamba wananunua kwa bei ya juu, tutachukua hatua.

“Lakini wakati tunachukua hatua napenda kuwakumbusha wateja wasikubali kuhujumiwa na wanafanyabiashara hao, wakatae kununua kwa bei hizo na kuwaripoti kwenye kampuni husika,” amesema.

Related Posts