MKUU wa wilaya ya Songwe mkoni hapa, Solomon Itunda ameagiza baadhi ya vijiji wilayani humo kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi (Sungusungu) ili kupunguza vitendo vya uhalifu vinavyosababisha mauaji hususani katika hasa kata ya Ngwala. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Itunda ameyasema hayo leo tarehe 28 Mei 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Ngwala ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya mkuu wa mkoa huo, Daniel Chongolo.
Ni baada ya wananchi wa kata hiyo kuomba ufafanuzi juu ya matukio ya mauaji katika kata yao.
Amesema alipokea taarifa za uwepo wa migogoro itokanayo na wafugaji wanaoingiza mifugo kienyeji na kuwa kero kwa wakulima hali inayosababishwa na baadhi ya viongozi wa vijiji wanaopokea rushwa na kuwapokea wafugaji pasipo ofisi yake kujua.
‘’Iseche kuna watu walijeruhimiwa na wafugaji, Ngwala mtu mmoja aliuawa, Mbangala na vijiji vingine nako kumekuwa na hali hii, mimi ni mwenyekiti wa kamati ya usalama, nakuhakikishia mkuu wa mkoa suala hili lipo chini ya uwezo wangu nitamaliza’’ amesema mkuu huyo wa wilaya.
Akiwa katika kijiji cha Iseche, Itunda amesema bonde la Iseche lina zaidi ya ng’ombe 10,000 ambazo wafugaji wamekuwa wakizichunga kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha vurugu.
Aidha, kutokana na matukio hayo, Mkuu wa mkoa huo, Daniel Chongolo amemuagiza mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua na kupelekwa mahakamani.
‘’Nakuagiza mkuu wa wilaya, hakikisha wahusika wote wanakamatwa, wakiwemo viongozi. Pia ni marufuku wenyeviti wa vijiji kuuza ardhi, kupokea wageni hasa jamii ya wafugaji kiholela bila kibali cha mkuu wa wilaya, pia fanya sensa ya mifugo itakayozidi irudishwe ilikotoka,’’ amesema Chongolo.