Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema Diaspora wana umuhimu mkubwa kutokana na mchango wao katika maendeleo ya Taifa kwani mwaka 2023, walituma fedha nyumbani kiasi cha Dola za Marekani 751.6 milioni (Sh 1.9 trilioni). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025 leo Jumanne bungeni jijini Dodoma, amesema kwa kuzingatia umuhimu wao, Serikali imejumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na Sera Mpya ya Ardhi ya 2024 na kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania ili kuwapa haki na upendeleo mahsusi.
Amesema Serikali itakamilisha mchakato huo wa hadhi maalumu katika mwaka ujao wa fedha kwa kuwa muswada wa mabadiliko ya sheria itakayokuwa na mabadiliko madogo ya sheria za uhamiaji na za ardhi ili hatimaye kuwezesha serikali kutoa hadhi maalumu.
“Lakini mwaka huu katika kalenda Bunge linaloendelea sasa Serikali itawasilisha muswada wa mabadiliko ya sheria itakayokuwa na mabadiliko madogo ya sheria za uhamiaji na za ardhi ili hatimaye kuwezesha serikali kutoa hadhi maalumu,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Makamba amesema Desemba mwaka 2023 wizara ilifanikisha Tanzania kusaini Mkataba wa Ubia baina ya Jumuiya za nchi za Afrika na Umoja wa Ulaya ambao utatumika kama nyenzo ya kisera na kisheria na kuratibu uhusiano wa Kiuchumi uliopo kati ya pande hizi mbili kwa miaka 20 ijayo.
“Mheshimiwa Spika utakumbuka kwamba nchi yetu imepata mafanikio makubwa sana kutokana na ushiriki wake wa mikataba ya aina hii,” amesema Makamba.