SAFARI ya Azam FC kuisaka nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao imefanikiwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Gold na kumaliza Ligi Kuu Bara ikiwa katika nafasi ya pili katika msimamo.
Azam FC iliyoanzishwa mwaka 2004 na kuanza kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2008, iliwahi kufanikiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja tu mwaka 2014 baada ya msimu wa 2013-2014 kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara.
Tangu mwaka 2014, Azam FC ilikuwa ikiisaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika lakini ikawa inajikuta ikiangukia Kombe la Shirikisho Afrika.
Chini ya Kocha Mkuu, Bruno Ferry na Msaidizi wake, Youssouph Dabo, Azam FC msimu huu imeishinda vita yake dhidi ya Simba na kumaliza nafasi ya pili kwa kukusanya pointi 69 nyuma ya mabingwa Yanga waliomaliza na pointi 80.
Azam FC walikuwa na vita kubwa na Simba ambao wote wamemaliza ligi na pointi sawa 69, lakini tofauti ya mabao manane ndiyo iliyowatenganisha na kuifanya Simba kumaliza nafasi ya tatu ambayo mara ya mwisho waliishika msimu wa 2015-2016 ikiwa pia ni nyuma ya Azam. Tangu 2015-2016, Simba haikuwahi kumaliza ligi nafasi ya tatu ambapo mara zote ilikuwa juu ya Azam.
Simba kumaliza kwao nafasi ya tatu, inawafanya msimu ujao kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilishuhudiwa mwaka 2018 wakishiriki michuano hiyo baada ya kuwa mabingwa wa Kombe la FA. Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara 22, wengi wameizoea kuiona ikitamba katika Ligi ya Mabingwa Afrika tofauti na Kombe la Shirikisho Afrika, huku timu hiyo ikiwa na rekodi ya kucheza robo fainali ya CAF mara tano.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania, alisema: “Sisi tulikuwa na uhitaji na JKT walikuwa na uhitaji wao, tumefanikiwa kupata ushindi wa mabao mawili lakini umetufanya tumalize nafasi ya tatu, hii imefika mwisho na imeshaonekana kila mmoja na nafasi yake.
“Tunaenda kipindi cha usajili baada ya ligi kumalizika, kuna vitu vitafanyiwa mabadiliko kwa sababu tunakwenda kwenye msimu mpya, hivyo tutarudi tukiwa imara zaidi.”
Mwneyekiti wa zamani wa Simba, Aden Rage, amesema: “Simba wasipaniki kwa kumaliza nafasi ya tatu na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika, wamsikilize kocha waliyenaye (Juma Mgunda) watafanikiwa tu msimu ujao kwani wana rekodi bora katika michuano ya CAF, wasione wamemaliza nafasi ya tatu wakawa wanyonge.
“Lakini pia nawapongeza Yanga kwa kumaliza mabingwa, ukiangalia wana wachezaji wazuri, wamefanya vizuri tangu mwanzo wa ligi, pia wana viongozi wazuri, kocha mzuri na mashabiki wazuri, nina imani msimu ujao wataendelea kufanya vizuri.”
Kocha wa Azam, Yossouph Dabo, alisema: “Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza ligi nafasi ya pili na kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, hii ni kubwa sana kwetu.”
Baada ya ligi kumalizika, namba mbili za juu Yanga na Azam zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, huku Simba na Coastal Union zikikata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kumaliza nafasi ya tatu na nne.
REKODI YA SIMBA KATIKA LIGI
2023/24 nafasi ya tatu pointi 69
2022/23 nafasi ya pili pointi 73
2021/22 nafasi ya pili pointi 61
2020/2021 bingwa pointi 83
2019/2020 bingwa pointi 88
2018/2019 bingwa pointi 93
2017/2018 bigwa pointi 69
2016/2017 nafasi ya pili 68
2015/2016 nafasi ya tatu 63
2014/2015 nafasi ya tatu 47
2013/2014 nafasi ya nne 38