Kisa Yanga… Kinzumbi aliamsha na Katumbi

WAKATI msafara wa maofisa wa Yanga ukijipanga kurudi tena kwa klabu ya TP Mazembe kuendeleza ushirikiano wao, ndani ya klabu hiyo bingwa  wa DR Congo winga wao ameliamsha rasmi.

Yule winga Philippe Kinzumbi ameliamsha rasmi akiwaambia mabosi wa klabu yake kiu yake kubwa ni kutaka kuja kucheza Tanzania bila kutajwa timu, lakini Mwanaspoti linajua akili zake zipo kwa Yanga.

Ipo hivi. Majuzi Kinzumbi alikutana na mabosi wa Mazembe waliomtaka kujadiliana naye juu ya ofa za klabu za Afrika Kaskazini, lakini mwenyewe akawagomea na kusisitiza ni heri kama kuna ofa kutoka Tanzania basi atakuwa radhi kucheza bila tatizo.

Mazembe imepokea ofa za maana za Kinzumbi kutoka Tunisia na Algeria, lakini winga mwenyewe amezigomea akiwasihi viongozi wake kama kuna ofa yoyote ya Ukanda wa Afrika Mashariki, basi atakuwa radhi kuliko kwenda Arabuni.

“Hataki kwenda Uarabuni anataka kuja Tanzania amesema kwenye kikao (Kinzumbi), ila ni kwamba hadi sasa hatuna ofa kutoka huko kwenu, lakini acha tuone kama atashawishika zaidi lakini ni ofa za Arabuni ni nzuri sana,” amesema bosi mmoja wa  Mazembe.

Yanga inataka kumsajili winga huyo wa kushoto mwenye uwezo wa kupangua ukuta wa timu pinzani baada ya kushindwa kuelewa kiwango cha Msauzi Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ na Mwanaspoti ina taarifa kwamba mabingwa hao wa Tanzania wanampigia hesabu na uhusiano wa ushirikiano baina ya klabu hizo huenda ukatumika kama njia ya kurahisisha dili hilo.

Majuzi mara baada ya taarifa hizo Mwanaspoti lilimtafuta Kinzumbi ambaye amekiri kuwajibu mabosi wake hana mpango wa kutaka kwenda kucheza Tunisia ama Algeria kukiwa na sababu alizowapa.

“Naheshimu mkataba wangu na Mazembe hata klabu ambazo zinanihitaji binafsi nimewaomba wazungumze na mabosi wangu wa Mazembe, japo natamani sana kuja kucheza Tanzania,” amesema Kinzumbi na kuongeza:

“Nataka kwenda kucheza sehemu ambayo nitapata furaha ya kuendeleza kipaji changu, nafahamu klabu inataka kupata fedha nyingi lakini kuna wakati unatakiwa kuangalia malengo yako kuliko pesa.”

Japo Kinzumbi ameshindwa kuweka bayana kama Yanga ilimfuata au la, lakini mtu wake wa karibu alisema wameulizia kama ana mkataba na wanataka kutumia fursa ya kuitembelea klabu hiyo baada ya awali mabosi wa Mazembe kuja Tanzania ili kujadili suala la mchezaji huyo aliyeisumbua timu msimu uliopita katika mechi za makundi za Kombe la Shirikisho Afrika, licha ya Mazembe kupasuka nje ndani kwa bao 1-0 na 3-1.
 

Related Posts