Mabadiliko ya tabianchi yalivyochochea majani vamizi nyanda za malisho

Arusha/Manyara. Safari kutoka Arusha hadi Kata ya Terrat wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara, ilichukua takribani saa mbili na nusu, licha ya umbali wa kilomita 84 tu.

Barabara ilikuwa mbovu na yenye vumbi jingi. Maeneo haya yanakaliwa na jamii za wafugaji.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Simanjiro ni kitovu cha shughuli nyingi za kiuchumi, ufugaji ukiwa kwa asilimia 80. Wafugaji wengi ni kutoka kabila la Wamasai. Nilikuwa na fikra kwamba maeneo hayo yameathiriwa na ukame hivyo kungekosekana majani lakini haikuwa hivyo, kwani majani yalikuwa yamestawi.

Hali hii ilinifanya kuuliza kulikoni?

“Haya ni magugu vamizi. Yanaitwa gugu karoti (Parthenium weed),” mwenyeji wangu Joshua Laizer alinijibu.

Nikahoji kupata ufahamu zaidi, akanieleza magugu hayo hayaliwi na mifugo japo yanastawi kwa kasi kwenye nyanda za malisho.

Kijijini Terrat, asubuhi nilikutana na Leboy Ngoira, mfugaji wa umri wa makamo aliyeanza uchungaji tangu utotoni, ambapo  ana zizi kubwa la ng’ombe lililozungushiwa miti mikavu yenye miiba. Kwa msaada wa vijana wawili, alikuwa akiandaa mifugo kwa ajili ya malisho.

Kwa kuliangalia, zizi hilo lina uwezo wa kuchukua zaidi ya ng’ombe 500, lakini walikuwapo chini ya 100.

“Sasa hivi hatufugi ng’ombe wengi. Tumepata maarifa ya kufuga wachache kwa ufanisi na kuwahudumia vizuri,” anasema Ngoira.

Anasema awali mifugo ilikuwa mingi, lakini kutokana na ukame maeneo ya malisho yamepungua au kutoweka, kutokana na maeneo mengi kuvamiwa na  magugu yasiyoliwa na mifugo.

Aliyataja magugu hayo kama Endelemeti kwa Kimasai (Ipomoea hildebrandtii) na mengine ni gugu karoti.

Katika boma lingine nilikutana na Lesira Samburi, aliyezungumzia kuhusu mimea vamizi.

“Ng’ombe hawali majani haya, na kwa sababu yanachanganyika na mengine, huenda yakaliwa kwa bahati mbaya. Wakila, wakati mwingine wanaugua na kutoa maziwa machungu,” anasema Samburi, ambaye ni kiongozi wa mila maarufu Laigwanani.

Utafiti kuhusu gugu karoti wa “Parthenium hysterophorus L. (Asteraceae) Kusini mwa Jagwa la Sahara, 2013” ulionyesha gugu karoti ni mmea vamizi kwenye maeneo yenye ukame.

Asili yake ni Amerika, hasa Mexico na kusini magharibi mwa Marekani. Utafiti huo ulionyesha mmea unaoathiri maeneo ya kilimo na malisho ya asili umeenea sehemu nyingi duniani.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), gugu karoti lilionekana kwa mara ya kwanza mwaka 2010 mkoani Arusha na baadaye kuenea Manyara, Kilimanjaro, Kagera na Geita, likiathiri maeneo ya kilimo, malisho na hifadhi za wanyamapori.

Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ilionyesha Simanjiro ina watu 291,169 waliotawanyika katika kata 18.

Wilaya hii ipo katika eneo la nusu jangwa, ikipata wastani wa mvua kati ya milimita 400 na 500 kwa mwaka. Hali hii ya hewa inatajwa ni rafiki kwa magugu vamizi.

Katika Kata ya Terrat, wakati fulani tulisafiri hadi dakika 10 bila kuona mimea mingine,  katika nyanda za majani ambayo awali ilikuwa eneo la malisho kwa mujibu wa mkazi wa eneo hilo, Justin Lukumay.

Kuna maeneo tulisimama kuangalia jinsi magugu hayo yalivyoenea kwa kasi. Kwa mtu mwenye urefu wa futi tano au sita, magugu hayo yanafika magotini hadi kiunoni. “Tulikuwa tunalisha mifugo hapa tulipokuwa watoto,” anasema Lukumay, ambaye ni mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Mpango wa Uhifadhi na Uwezeshaji Jamii Tanzania (TACCEI) lililoko Simanjiro.

Utafiti wa mwaka 2022 uliofanywa na wasomi watano kutoka Tanzania na Kenya ulionyesha magugu vamizi anaathiri sana spishi za majani asili.

Utafiti ulionyesha maeneo yaliyoathiriwa  zaidi, asilimia 43 ya spishi ni gugu karoti, ambayo ni kubwa zaidi na majani ya Eleusine indica (Kisesehunda) yalifuata kwa asilimia 25.

Katika maeneo yaliyoathiriwa kidogo, mmea ulitawala kwa asilimia 36.2, ikifuatiwa na asilimia 7.9 ya spishi nyingine. Katika maeneo yasiyoathiriwa, gugu karoti ilikuwa asilimia 3.7.

Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Simanjiro, Dastan Mdolwa anasema, “magugu yalianza polepole kijijini Terrat, lakini sasa yameenea karibu robo tatu ya wilaya nzima.

Mwenyekiti wa kamati ya gugu karoti Arusha, Ndelekwa Kaaya anasema:

“Tunavyochelewa, ndivyo linavyoenea zaidi,  linakuwa mahali popote na mimea ya eneo hilo inaathiriwa. Unaweza kupata chini ya asilimia 30 ya kile unachoweza kuvuna.”

Nikiwa ziarani wilayani Monduli, mkoani Arusha, niliyaona magugu haya, ingawa si kwa wingi kama Simanjiro.

Monduli ni miongoni mwa wilaya kame nchini. Ina hali ya hewa ya joto katika maeneo ya chini na baridi maeneo ya juu. Wastani wa mvua ni milimita 500 hadi 900 mtawalia.

Wakazi wake wanajishughulisha na shughuli kadhaa za kiuchumi kama vile ufugaji, kilimo na uhifadhi wa wanyamapori.  Ina watu 227,585, zaidi ya asilimia 90 wakiwa wafugaji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Terrat, Kone Dedukenya, anasema wameamua kutenga maeneo ya malisho na kuyahifadhi.

“Mwaka jana, kwa kushirikiana na halmashauri, walitenga maeneo kwa ajili yetu ambayo tumeainisha na watu hawaruhusiwi kuchunga huko,” anasema.

Eneo tulilotembelea limezungukwa na uzio wa waya likiwa na ukubwa wa mita za mraba 160,000 (takriban ekari 40), kwa mujibu wa Msimamizi wa Kamati ya Malisho, Terrat, Stephano Kabuni.

Eneo hilo halina nyasi nyingi, lakini ni bora ikilinganishwa na nje ya uzio.

“Tuliondoa magugu vamizi na kupanda nyasi za asili,” anasema Kabuni.

Anasema kuna maeneo mengine manne kama hayo yaliyotengwa kwa ajili ya utafiti.

Akizungumza historia ya magugu vamizi, anasema tangu mwaka 2019 katika eneo la ekari 715 waliondoa magugu vamizi ya indelemeti lakini walishindwa kudhibiti gugu karoti.

“Unapoondoa gugu karoti, mbegu zake hazipotei hata mmea ukiwa mbichi na huendelea kuota. Tumeshindwa kudhibiti,” anasema.

Katika Kijiji cha Losirwa, Monduli wameweka maeneo ya malisho pia, lakini tofauti na Terrat, huko nyasi zinaonekana kustawi.

Yamati Laizer, Mwenyekiti wa kijiji hicho anasema kuna vikundi 12 vya wanawake wanaoshiriki kazi ya kupanda nyasi na shughuli nyingine za kuboresha hali yao kiuchumi na kupunguza utegemezi.

Kiongozi wa kikundi cha wanawake 30 wafugaji, Grace Narumuta, anasema walipata mafunzo ya kupanda na kuhudumia nyasi mwaka 2023. “Tulielimishwa na Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), tumepanda nyasi kama unavyoona zimekua vizuri. Siku ya Kimataifa ya Wanawake, tulivuna mbegu na kuziuza kwa vikundi vingine,” anasema.

Grace anasema wamedhibiti majani vamizi na sasa wanapata fedha, hivyo wanahama kutoka shughuli hatarishi kwa mazingira kama vile kuuza mkaa na kuni.

Meneja wa mradi wa PWC Monduli, Stella James, anasema,  “wanawake katika jamii hii tumekuwa tukiachwa nyuma, hivyo kutambua hili shirika letu liliona umuhimu wa kuwasaidia kupunguza utegemezi. Tumewasaidia katika masuala mengi ikiwemo kupanda nyasi.”

Suluhisho, msimamo wa Serikali

Utafiti kuhusu gugu karoti unapendekeza mbinu za usimamizi wa magugu zilizoendelezwa zikijumuisha njia za kitamaduni, mitambo, kemikali na za kibiolojia kutumika kudhibiti uvamizi.

Mwenyekiti Kaaya anasema wanawafundisha wananchi kuhusu gugu karoti akipendekeza suluhisho ni kuyang’oa na kuyachoma kwa uangalifu.

Mtafiti wa visumbufu vya mimea kutoka TPHPA, Ramadhan Kilewa anasema wamepitisha Mbinu Jumuishi ya Kudhibiti Wadudu (IPM) katika kudhibiti, ikijumuisha njia ya kibiolojia kwa kutumia wadudu maalumu wanaokula gugu karoti bila kuathiri mimea mingine.

“Njia ya kung’oa mimea iliyoathiriwa na kuichoma pia hutumika na nyingine ni pamoja na kemikali maalumu zinazotumiwa kuangamiza mmea bila kuathiri mingine,” anasema.

Hata hivyo, anasema mbinu zote hutegemea aina ya eneo, akibainisha huwezi kutumia njia za kemikali katika maeneo ya malisho au hifadhi za wanyamapori kwa sababu wanyama wakila mimea yenye sumu watakufa, lakini njia ya kibiolojia ni suluhisho kwa maeneo hayo.

TPHPA inaendelea kusambaza na kutoa elimu katika maeneo yaliyoathiriwa, akisema hatua zinazochukuliwa zinatoa tumaini.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Faki Lulandala, anasema wanaendelea kushughulikia tatizo la gugu karoti na kutafuta suluhisho la kudumu.

Imefadhiliwa na Bill & Melinda Gates Foundation.

Related Posts