Makamba ataja faida 10 ziara za viongozi nje

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024, wizara hiyo iliratibu ziara 31 za viongozi wakuu wa kitaifa nje ya nchi na kuleta manufaa mbalimbali nchini ikiwamo kufungua milango ya kiuchumi kupitia uhusiano wa kimataifa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Pia amesema wizara hiyo iliratibu ziara 12 za kikazi za Makamba katika mataifa mbalimbali kuliletea maendeleo Taifa kama vile kuimarisha uhusiano wa Tanzania na nchi marafiki na taasisi za kimataifa.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi  ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025 bungeni jijini Dodoma, Makamba amesema ziara hizo zimeiwezesha Tanzania kusaini mikataba na makubaliano ya ushirikiano (MOUs) 78 katika sekta mbalimbali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwenyeji wake Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan mara baada ya kuwasili katika lkulu ya Kulliye
Ankara nchini Uturuki tarehe 18 Aprili 2024.

Pia zimewezesha upatikanaji wa nafasi za masomo kwa Watanzania, upatikanaji wa fursa za ajira kwa Watanzania katika nchi mbalimbali, upatikanaji wa soko la mazao kwa wakulima, upatikanaji wa fedha za miradi ya kimkakati kwa mfano reli ya kisasa (SGR) na Bandari ya Mangapwani, Zanzibar.

“Zimevutia uwekezaji kiasi cha kufikia miradi yenye thamani ya dola za Marekani 5.7 bilioni kwa mwaka 2023. Pia zimeipa Tanzania fursa kuongoza mijadala ya kidunia yenye maslahi kwa nchi yetu, kuvutia watalii kuja kutembelea Tanzania baada ya kupata taswira nzuri ya nchi yetu kupitia ziara za viongozi wetu na wataalamu wa Tanzania kutoka Vyuo Vikuu na Taasisi.

“Pia kupata fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu na wenzao wa nchi mbalimbali kupitia makubaliano yanayowekwa kwenye ziara hizo,” amesema Makamba.

Related Posts