Mwanafunzi anayedaiwa kulawitiwa na mwalimu mkuu kuhamishwa shule

Musoma. Hatimaye mwanafunzi anayedaiwa kubakwa, kulawitiwa na kisha kunyweshwa sumu na mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Masaunga wilayani Bunda,  anatarajiwa kuhamishiwa katika shule nyingine ili kuendelea na masomo.

Mwanafunzi huyo wa darasa la sita amepata fursa hiyo kufuatia habari iliyoandikwa na mitandao ya Mwananchi, akiiomba Serikali pamoja na wadau kumuwezesha kuhamishwa shule,  kutokana na mazingira yaliyopo kwa sasa kutokuwa rafiki kutokana na tukio hilo.

Akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake leo Mei 28,2024, Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mara, Kinyemi Sepeku,  amesema taratibu zote za uhamisho zimekamilika hivyo mwanafuzi huyo anatarajiwa kuanza masomo katika shule hiyo mpya baada ya shule kufunguliwa  Julai mwaka huu.

“Tunamuondoa kabisa katika mazingira ya pale, atakwenda shule ya bweni na tumeona kuwa muhula wa kwanza unaishia ngoja amalize mitihani yake ila shule zikifunguliwa tu ataanza masomo rasmi kwenye hiyo shule alikohamishiwa,” amesema.

Hata hivyo, Sepeku hakutaka kutaja jina la shule hiyo kwa sababu za kimaadili kwa maelezo kuwa kufanya hivyo,  kutasababisha mwanafunzi huyo aweze kutambulika na kuendela kupata wakati mgumu katika masomo yake.

Amesema uamuzi wa kumuhamishia mwanafunzi huyo katika shule nyingine, unalenga kuhakikisha anapata mazingira mazuri ya kujifunza na kusomea kutokana na mazingira yake ya awali kutokuwa rafiki tena  kufuatia tukio hilo..

Mbali na uhamisho huo,  mwanafunzi huyo  pia tayari amempata msamaria mwema aliyejitolea kuishi naye   nyakati za likizo ili kuepuka kurudi kijijini kwao alikotendewa tukio hilo.

Msamaria huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe, amesema ameamua kumchukua mwanafunzi huyo na kuishi naye kwake huku akimpa mahitaji muhimu yakiwemo ya shule,  baada ya kubaini kuwa hata mazingira ya nyumbani kwao sio salama kwake.

Mama wa mwanafunzi huyo amesema tayari msamaria huyo amefika nyumbani kwake na kufanya mazungumzo pamoja, ambapo wamekubaliana mwanafunzi huyo atakwenda nyumbani  kwa msamaria huyo muda mfupi kabla shule hazijafunguliwa.

Mwalimu Vicent Nkunguu anadaiwa kumbaka na kumlawiti mwanafunzi huyo kisha kumnywesha sumu kwa lengo la kupoteza ushahidi  kati ya Machi 8 na 9 mwaka huu.

Matukio hayo yanadaiwa  kutokea nyumbani kwa mwalimu huyo ambapo mwanafunzi huyo alikwenda kwa ajili ya kuwapikia watoto wa mwalimu huyo kutokana na mke wa mwalimu kwenda kijiji jirani kwa ajili ya ibada.

Tayari mwalimu Nkunguu amefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Bunda akikabiliwa na mashtaka matatu ya kubaka, kulawiti na  kujaribu kuua  kinyume cha sheria.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mahakamani hapo Juni 12 mwaka huu.

Related Posts