Serikali kuwapa hadhi maalumu Diaspora

Dodoma. Serikali imesema ipo katika hatua za kukamilisha kutoa hadhi maalumu kwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania,   ambapo muswada wa marekebisho ya sheria utawasilisha katika Bunge hili.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Mei 28, 2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha Sh241.069 bilioni ambapo kati ya fedha hizo Sh229.4 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh11.6 bilioni ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

Maombi hayo ya fedha ni pungufu kwa asilimia tatu ikilinganishwa na bejeti iliyopita na hiyo imetokana na kupungua kwa fedha za maendeleo kwa asilimia 34.

Kauli ya Serikali ya kutoa hadhi maalumu kwa Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine kwa kuukana wa awali, imekuja baada ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kueleza nia ya Serikali ya kutoa hadhi maalumu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa wakati huo, Dk  Stergomena Tax  alilieleza Bunge kuwa wizara yake ilikuwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwapatia hadhi maalumu diaspora wenye asili ya Tanzania na uraia wa nchi nyingine, ili kuwawezesha kuchangia miradi ya kitaifa.

Kauli ya Dk Tax ilitokana na hoja za wabunge waliokuwa wakidai uraia pacha, huku siku kabla ya bajeti ya wizara hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alikuwa ametoa maelezo bungeni kwamba  kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura ya 357 Rejeo la 2002, wote walioukana uraia wa Tanzania wanapoteza haki ya kuendelea kuwa Watanzania.

Leo, Makamba amezungumzia mchango wa diaspora ambao ni raia wa Tanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine kwamba Serikali imetambua mchango wa raia na hivyo itawasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya sheria kuwapa hadhi maalumu.

“Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimuwa diaspora, Wizara imeendelea kushiriki katika kuweka mazingira wezeshi yakiwemo ya kisera na kisheria kama hatua muhimu ya kuchochea ushiriki wa Watanzania waishio nje ya nchi na raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania katika maendeleo ya Taifa.

“Hatua hizi ni pamoja na kujumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na kutoa hadhi maalum kwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania ili kuwapa haki na upendeleo mahsusi,” amesema.

Related Posts