Simba yakwama kwa kocha Mhispaniola

UONGOZI wa Simba umeshindwa kumshawishi kocha wa makipa wa timu, Mhispania Daniel Cadena kuendelea kubaki baada ya kuandika barua ya kutimka Msimbazi.

Cadena ambaye alitaja sababu za kuondoka ndani ya timu hiyo kuwa ni kuhitaji kuwa karibu na familia yake amemalizana na timu hiyo na leo anakamilisha majukumu yake kwenye mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya JKT Tanzania.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeiambia Mwanaspoti kuwa kocha huyo tayari ameandika barua ya kuomba kuondoka baada ya makubaliano ya pande mbili kushindwa kufikia muafaka.

“Ni kweli Cadena katupa barua ya kuomba kuondoka na ni suala la muda tu kwake kutimka ndani ya timu hii ni baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kumtaka kocha huyo aendelee kusalia ndani ya timu,” kimesema chanzo hicho na kuongeza:

“Mwanzo alitueleza kuwa anataka kuondoka tuliomba mazungumzo naye ili tuone kama tunaweza kumshawishi aendelee kubaki lakini mambo yamekuwa magumu msimamo wake ni uleule anataka kuondoka.”

Mwanaspoti lilimuuliza juu ya mkataba wake ndani ya timu hiyo chanzo hicho kilikiri kuwa mkataba wake unaisha mwisho wa msimu.

“Alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Simba wenye kipengere cha kuongeza mwingine ila yeye mwenyewe ameonyesha kutokuwa na utayari wa kuendelea nasi kwa msimu ujao japo tumepambana kwa ajili ya kumbakisha imeshindikana,” kimesema chanzo hicho.

Cadena alipotafutwa kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo, amesema kwa sasa hana nafasi ya kuzungumza kuhusiana na suala la mkataba na akili yake ameielekeza kumalizia mechi ya ligi iliyobaki.

“Tunamaliza msimu na kibarua changu ndani ya Simba kinaishia hapo kwa mujibu wa mkataba. Nafikiri kama kutakuwa na mabadiliko yoyote juu ya mimi kuendelea au kuondoka itajulikana na nitakuwa na wakati mzuri wa kuzungumza,” amesema.

Related Posts