Simulizi machungu ya kukosa elimu kwa wasichana Geita, kisa ndoa za utotoni

Ni takribani umbali wa kilomita 35 kutoka Geita mjini, ikichukua takribani dakika 50 kwa msafara wa wadau wa elimu kuwasili katika sekondari ya Bung’wangoko ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Juma la Kimataifa la Elimu (GAWE) yaliyofanyika mkoani Geita.

Kama ilivyo ada ya Waafrika mgeni anapofika anakaribishwa kwa ukarimu, hivyo ndivyo ilivyofanyika kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo waliwapokea wageni kwa shangwe na vigelegele na burudani mbalimbali.

Kati ya burudani nyingi zilizotolewa igizo la wanafunzi liligusa hisia za wengi, hasa katika nafasi ya mhusika mkuu iliyochezwa na Elizabeth Ernest mwanafunzi wa kidato cha kwanza.

Maudhui ya igizo hilo lilikuwa ni mimba na ndoa za utotoni namna inavyowaathiri watoto wa kike katika jamii ya Wasukuma ambao ndiyo wenyeji wa mkoa wa Geita.

Kujiamini kwake na uwezo wake wa kujielezea kwenye hadhira hasa katika jamii iliyotawaliwa na mfumo dume, ilionesha dhahiri kuna kitu cha ziada ndani ya binti huyu.

Nilipokaa naye chini na kuzungumza naye ndipo nilipobaini kwamba nilikuwa sahihi, binti huyu ni miongoni mwa wasichana wenye kiu kubwa ya kupata elimu na yuko tayari kufanya lolote kutimiza lengo lake. “Huwa nafurahi nikiwaona watumishi wakiwa wamependeza wanaenda kazini, naamini hata mimi naweza kuwa kama wao ndiyo maana naweka nguvu darasani kwa kuwa naamini njia pekee itakayoniwezesha kufanikisha hilo elimu,” anasema Elizabeth.

Binti huyu wa miaka 18, ni miongoni mwa wasichana waliokumbana na msukumo wa kuoelewa wakiwa na umri mdogo lakini alifanikiwa kuvuka kiunzi hicho.

 Elizabeth alifanikiwa kukimbia na kukwepa kuozeshwa lakini taarifa zinaonesha kuwa wapo wasichana katika mkoa huo ambao walilamizishwa kukatisha masomo na kutakiwa kuolewa.

 Baada ya kumaliza darasa la saba akiwa na miaka 11, familia yake ikapanga mpango wa kumuozesha kwa mmojawapo wa wazee katika kijiji anachoishi, kutokana na kile kilichoaminika kwamba safari yake ya elimu imeishia hapo kinachofuata ni kuanzisha familia.

Elizabeth hakukubaliana na uamuzi huo kwa kuwa aliamini ndoto zake haziwezi kutimia endapo angekubali kuolewa, hilo likamsababishia kutoroka nyumbani.

“Sikukubaliana na uamuzi wa kuolewa nilikuwa mdogo kiumri ingawa kimuonekano nilionekana mkubwa, sikukubali kwa sababu niliamini nina safari ndefu ya elimu ili kutimiza ndoto zangu.Nikafikia uamuzi wa kutoroka kwenda Mwanza. Kwa kutumia fedha za ujira niliopata kutokana na vibarua vya kulima nilifanikiwa kupata nauli iliyonifikisha Mwanza.

“Si kwamba nilikuwa nafahamu naenda wapi na kufanya nini, ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika Mwanza na nilipofika stendi sikuwa na uelekeo. Nilikutana na mwanafunzi nikamsimulia mkasa wangu akaniambia niende nyumbani kwao,”anasema Elizabeth.

 Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya ya binti huyu, aliishi kwenye familia hiyo mpya hadi pale walipomtafutia kazi za ndani jijini Mbeya.

 Uchapakazi na uaminifu mkubwa alioonesha kwa bosi wake ulimfanya kumpandisha kutoka mfanyakazi wa ndani hadi kuwa mhudumu wa dukani.

“Yule bosi wangu alikuwa mama mwenye upendo, alivutiwa na namna ninavyofanya kazi akajenga uaminifu mkubwa kwangu, haikuchukua muda mrefu akaniingiza ndani kwenye sehemu ya fedha nilifanya kazi yangu kwa ufanisi mkubwa,”.

Baada ya kukaa nje ya mfumo wa elimu kwa takribani miaka minne, hatimaye siku moja alifika mteja ambaye aliguswa na uwezo wake kiakili na kuanza kumhoji.

 Anasema,”Kuna mzee mmoja alikuwa anakuja dukani, siku moja akaanza kunihoji kwa nini nipo hapo na sio shuleni nikamueleza mkasa niliopitia na alionekana kuguswa, akaanza kuniambia kuhusu tamko la Serikali la kuwaruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni.

 Akawa ananionesha video mtandaoni na kuniuliza kama naweza kurejea shuleni na kunishawishi nirudi nyumbani.Nikamwambia niko tayari na akanilipia ada nisome masomo ya ziada kabla ya kurudi shuleni.”.

Huo ukawa mwanzo mpya wa maisha ya Elizabeth, baada ya kujengwa kifikra, mzee huyo alimsaidia pia kupata nafasi katika shule ya msingi kwa kurudia darasa la sita akiwa na miaka 16.

 Haikuwa rahisi kwa jamii kumpokea Elizabeth hasa kutokana na umri wake kutoendana na mwanafunzi wa darasa la sita, alikutana na kila aina ya udhalilishaji na kukatishwa tamaa.

Anasema: “Nilikuwa naambiwa maneno ya kukatisha tamaa kwamba umri na muonekano wangu haustahili kuwepo shuleni. Natakiwa niolewe lakini kwa kuwa nilifahamu lengo langu ni lipi sikuwayumbishwa na maneno hayo.

“Niliendelea na shule hatimaye nikamaliza elimu ya msingi nikiwa na miaka 17 na nikafanikiwa kufaulu vizuri, nilipata A tano na B mbili nikachaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Bung’wangoko,”.

Januari 2024 akaanza safari yake ya elimu ya Sekondari akiwa na hofu ya namna atakavyopokelewa lakini bahati ilikuwa upande wake walimu na wanafunzi wenzie walimpokea vyema.

 Changamoto pekee ambayo amebaki nayo ni namna jamii inavyomtazama na kuendelea kumkatisha tamaa kwamba umri wake hatakiwi kuchangamana na wanafunzi wengine bali aolewe.

“Wananiambia mimi ni mzee sitakiwi kujichanganya na wanafunzi, sehemu pekee ninayotakiwa kuwepo ni kwenye ndoa, sikubaliani na wanachokisema na ndiyo sababu sijali nasimamia kile ninachokiamini.

“Nataka kuwa muuguzi wa hospitali, naamini ili kutimiza ndoto hiyo ni lazima nisome hivyo hakuna namna naweza kuacha shule kwa sababu ya maneno ya watu, nitasoma na nitahitimu masomo yangu,”.

Shauku hiyo inamsukuma Elizabeth kuwasihi wasichana wengine kutokubali kukatishwa tamaa kwa namna yoyote ile na badala yake wasimamie ndoto zao kwa kuweka kipaumbele kwenye elimu.

Mkuu wa shule amzungumzia

Akimzungumzia mwanafunzi huyo, Mkuu wa shule ya sekondari Bung’wangoko Jackson Barnabas anamtaja Elizabeth miongoni mwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa kitaaluma.

“Anafanya vizuri darasani, kwa kifupi ni mwanafunzi ambaye anafundishika na kuelewa anachofundishwa ndani ya muda mfupi, ingawa tunaona kuna changamoto anazokutana nazo nyumbani.

“Kwenye jamii ya Kisukuma mwamko wa elimu uko chini hasa kwa watoto wa kike, hivyo kuna mazingira ambayo anakutana nayo kwa namna moja au nyingine yanampa vikwazo ila anapambana,”.

Hilo linaelezwa pia na Mariam Mkerewe mkazi wa kijiji cha Mgusu mkoani humo, mama huyu anaeleza kuwa kukosa mwamko wa elimu kunawafanya wazazi wengi kuwa tayari kuozesha watoto wao.

 Anasema wazazi wengi kipaumbe chao ni mali hivyo hutumia muda mwingi kwenye shughuli za uzalishaji mali na wapo ambao wanaona mtoto wa kike ni mtaji.

“Tukiamka kila mmoja anashika njia yake ya kujitafutia, hatuna muda wa kukagua daftari wala kufuatilia maendeleo ya mtoto sasa kwa mtindo huu unafikiri unawezaje kumthibiti.

 Wapo ambao hawaamini kabisa katika elimu hasa kwa mtoto wa kike ndiyo hao ambao wako tayari kumwambia watoto wafanye vibaya kwenye mitihani ya mwisho ili wawatumikishe na kuwaozesharifa,” anasema Mariam.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Mgusu iliyopo halmashauri ya Geita vijijini, Mwadawa Ghati anasema mbali na msukumo wa kuolewa, wanafunzi wengi wanakatisha masomo kwa sababu ya umaskini wa familia. “Inawezekana mwanafunzi anataka kusoma lakini mazingira ya nyumbani hayamruhusu, utakuta wazazi wanaondoka bila kuacha chochote nyumbani hivyo inabidi ajitafutie chakula, hapo ndipo anapoona ni heri asiende shule akatafute kipato.

“Kingine ninachokiona kuna ushawishi mkubwa unaofanywa na wachimbaji kule kijijini, kwa kuwa wao wana fedha ni rahisi kuwashawishi wasichana na hatimaye wanaacha shule na kutokomea nyumbani,” anasema Mwadawa.

Akizungumzia hilo Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) Martha Makala aliwataka wazazi wa jamii hiyo kuweka kipaumbele cha elimu kwa watoto bila kubagua jinsia.

“Suala la elimu halina mbadala na haitakiwi kuwa ya kundi moja, watoto wote wanapaswa kupata elimu. Jitihada nyingi zinafanyika ikiwemo ujenzi wa miundombinu, mpango wa elimu bila ada hii yote ni kutoa fursa watoto wote wapate elimu.

Kuendeleza mila potofu za kuwaozesha mabinti au kuwaacha katika mazingira hatarishi yatakayowafanya warubuniwe ni jambo lisilokubalika, wasichana nao wana haki ya kupata elimu na sisi kama wazazi tunapaswa kulisimamia hilo tena wasome katika mazingira wezeshi na rafiki,” anasema Martha.

Takwimu zinaonesha katika mwaka wa masomo 2024, wanafunzi 52438 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini hadi kufikia Machi 29 wanafunzi 46,138 sawa na asilimia 88 ndio walioripoti shuleni.

Related Posts