Dodoma. Serikali kwa mwaka wa fedha ujao, umepanga kujenga majengo ya kiuchumi katika majiji ya Kinshasa (DRC- ghorofa 25) na Nairobi (Kenya- ghorofa 22).
Picha za majengo ya Nairobi na Kinshasa zipo tayari na picha za majengo mengine ya kitega uchumi katika majiji ya Maputo (Msumbiji), Bujumbura (Burundi), Kigali (Rwanda) na Lilongwe (Malawi) nayo imewekwa wazi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Mei 28, 2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha Sh241.069 bilioni ambapo kati ya fedha hizo Sh229.4 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh11.6 bilioni ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.
Maombi hayo ya fedha ni pungufu kwa asilimia tatu ikilinganishwa na bejeti iliyopita na hiyo imetokana na kupungua kwa fedha za maendeleo kwa asilimia 34.
Kwa mujibu wa Makamba, Serikali ina nyumba na viwanja 109 dunaini kote na kodi ya pango wanayolipa ni Sh29 bilioni kwa mwezi.
Amesema uwekezaji huo ukikamilika utaingiza Sh36 bilioni kwa mwezi na kwa mwaka Sh692 bilioni.
“Wizara imeingia nakubaliano ya ubia na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Nairobi.
Amesema mradi huo unahusu kuendeleza kiwanja kilichopo katika eneo la Upperhill jijini Nairobi kwa kujenga majengo pacha ya ghorofa 22.
Makamba amesema Wizara imekamilisha taratibu za kisheria za makabidhiano ya nyaraka na kuhamisha rasmi majukumu ya ujenzi wa mradi kwenda NSSF.
“Wizara pia kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), imekamilisha maandalizi ya nyaraka za kisheria kwa mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi Kinshasa DRC.
“Utekelezaji wa mradi huo unafanyika katika kiwanja cha ubalozi kilichopo mtaa wa Boulevard de 30 Juin jijini Kinshasa ambapo utahusisha ujenzi wa jengo la ghorofa 25.
Amesema pia Wizara inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya majengo ya Wizara pamoja na vitega uchumi katika viwanja vya Serikali vilivyopo.